Yahya Jammeh akausha makasha yote Gambia | Magazetini | DW | 27.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Yahya Jammeh akausha makasha yote Gambia

Yahya Jammeh akimbilia uhamishoni Guine ya Ikweta, Christian Wulff avishwa jokho la balozi wa Afrika katika majukwaa ya kimataifa na adha Afrika Kusini ni miongoni mwa mada magazetini wiki hii

 

Tunaanzia Afrika Magharibi, nchini Gambia ambako mtawala wa zamani Yahya Jammeh amekubali hatimae kuwenda uhamishoni na kumwachia uwanja rais mpya Adama Barrow kuiongoza nchi hiyo  ndogo ya Afrika Magharibi. Hali hiyo imewezekana kutokana na juhudi za jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS. "Wamemkubalia mengi mno" ndio kichwa cha habari cha gazeti la die Tageszeitung lililomnukuu rais mpya Adama Barrow akilalamika. Die Tageszeitung linawataja waandishi habari waliokuwepo karika uwanja wa ndege wa Banjul Jammeh alipokuwa akiondoka; masanduku yasuiyokuwa na idadi yalipaakizwa ndani ya ndege hiyo na ndege maalum ya mizigo ikaletwa kutoka Chad ili kusafirisha magari 13 ya anasa. Jammeh ameondoka na kila kitu ambacho katika kipindi cha miaka 23 ya utawala wake aliweza kukipatia. Die Tageszeitung linaashiria mvutano uliozuka kati ya wapatanishi wa jumuia ya ECOWAS na rais mpya wa Gambia. Yadhihirika kana kwamba waüatanishi hao ndio waliomkubalia Jammeh atwae kila alichotaka kutwaa.

Jammeh hana wasi wasi wa kukamatwa akiwa Guinee ya Ikweta

"Makasha matupu" ndio pia kichwa cha maneno cha gazeti la Frankfurter Allgemeine linalojiuliza kama kweli Yahya Jammeh hajabakisha chochote nchini humo. Gazeti linamnukuu mshauri wa karibu wa rais mpya Adama Barrow, Mai Fatty akisema Yahya jammeh sio tu ameondoka na magari yote ya fakhari ya serikali, bali pia makasha ya benki kuu ya Gambia ameyaacha matupu. Kwa mujibu wa Fatty, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, Euro milioni kumi zilihamishiwa ng'ambo toka akkonti ya benki kuu ya Gambia. Chaguo la Jammeh kuhamia Guine ya Ikweta na tuhuma za hivi karibuni za kuiba mali ya umma, yote hayo ni mtihani kwa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine linalokumbusha kwamba taasisi hizo zimeahidi Jammeh akikubali kuondoka, milki yake,  ya jamaa zake, wafuasi wake na ya chama chake hazitaguswa. Frankfurter Allgemeine linasema hata kama jumuia hizo tatu zitaamua kumwandama kisheria Jammeh kwa ufisadi, hata hivyo juhudi zao hazitafanikiwa kwasababu Guine ya Ikweta haiitambui korti ya kimataifa ya uhalifu: kwa maneno mengine, linamaliza kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine labda Jammeh atasumbuliwa pengine na mbu wa Malaria  wa Guine ya Ikweta, lakini sio mahakama ya kimataifa ya uhalifu.

Christian Wulff apiganie usahirikianao wa Ulaya na Afrika

 Christian Wulff akabidhiwa upya jukumu la upatanishi-safari hii kama balozi wa Afrika, linaandika gazeti la Süddeutsche linalosema miaka mitano baada ya kujiuzulu kama rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani, Christian Wulff tangu miaka miwili iliyopita amegundua uwanja mwengine wa majukumu unaomrejesha katika majukwaa ya kimataifa kama mpatanishi kati ya Ulaya na Afrika. Süddeutsche linazungumzia mkutano ulioitishwa  jumatatu iliyopita mjini Berlin na kuhudhuriwa na wawakilishi wa sekta ya kilimo kutoka kila pembe ya dunia. Christian Wulff pia anadai pawepo mpango maalum  mfano wa ule wa Marshall Plan ulioandaliwa na Marekani kwaajili ya Ujerumani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia."Matatizo ya Afrika ni ya Ulaya pia" anasema mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Democratic Union."Ulaya inabidi ishirikiane na Afrika" anasema Christian Wulff anaeshauri Ujerumani inaweza kukamata nafasi ya mbele hasa kwakua ndio mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya mataifa 20 yaliyoendelea kiviwanda na yale yanayoinukia G-20.

Adha katika viwanja vya ndege vya Afrika Kusini

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Afrika Kusini ambako Frankfurter Allgemeine linasema ni udhia mkubwa mtu akitaka kusafiri na mtoto mdogo nchini humo.Watu ,mamoja raia au watalii wanazuwiliwa kuondoka ikiwa cheti hiki au kile  kinachomhusu mtoto kinakosekana. Adha za uwanja wa ndege na ripoti za watoto wadogo wanaohanikiza kwa vilio au watalii wanaokataliwa kuondoka yote hayo yanaathiri sekta ya utalii ya Afrika kusini linamaliza kuandika Frankfurter Allgemeine.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com