1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Xi: Uhusiano kati ya China na Urusi ni wa 'thamani kubwa'

15 Aprili 2026

Rais wa China Xi Jinping amesema kwamba utulivu na uhakika wa uhusiano wa China na Urusi ni wa thamani hasa katika mazingira ya kimataifa yanayoambatana na mabadiliko na machafuko.

https://p.dw.com/p/5CCIs
Xi Jinping alikmaribisha waziri wa mambo ya nje wa Urusi Serge Lavrov mjini Beijing
Rais wa China Xi Jinping amesema utulivu na uhakika wa uhusiano wa China na Urusi ni wa thamani hasa katika mazingira ya kimataifa Picha: China Daily/REUTERS

Akizungumza Jumatano wakati wa mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, huko Beijing, Xi amesema mwaka huu unaadhimisha miaka 30 ya ushirikiano wa kimkakati wa China na Urusi na kumbukumbu ya miaka 25 ya Mkataba wa Ujirani Mwema na ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Urusi.

"Chini ya mwongozo wa kimkakati wa mimi na Rais Putin kwa miaka mingi, ushirikiano wa kimkakati wa kina wa China na Urusi umedumisha maendeleo ya kiwango cha juu na matokeo ya ushirikiano yenye matunda katika nyanja mbalimbali. Katika mazingira ya kimataifa yaliyojaa mabadiliko na machafuko, utulivu na uhakika wa uhusiano wa China na Urusi ni wa thamani sana, na uhai mkubwa na umuhimu wa mfano wa mkataba wa ujirani mwema na ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Urusi ni muhimu zaidi."

Rais Xi amesema China na Urusi zinahitaji kutumia ushirikiano wa kimkakati wa karibu na wenye nguvu ili kutetea maslahi halali ya mataifa yote mawili na kulinda umoja wa nchi za kusini mwa dunia.

Mkutano kati ya Xi na Sanchez
Rais Xi Jinping wa China na Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez walihudhuria mkutano mjini Beijing mnamo Aprili 14, 2026.Picha: Haruna Furuhashi/REUTERS

Pia ametoa wito kwa nchi hizo mbili kuonyesha uwajibikaji na kujitolea kwa mataifa makubwa na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Lavrov anajiunga na Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, Mwanamfalme wa Abu Dhabi, Sheikh Khaled bin Mohamed bin Zayed Al Nahyan, na kiongozi wa Vietnam, To Lam, katika mkutano na Xi wiki hii.

Uhusiano kati ya China na Urusi umeimarika zaidi katika miaka ya hivi karibuni, hasa kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mapema mwaka wa 2022. Mtazamo usio wa kawaida wa Trump kuhusu vita nchini Ukraine umeongeza mabadiliko katika uhusiano huo lakini hauonekani kuubadilisha kimsingi.

Putin alipotembelea China mnamo Septemba, Xi alimkaribisha mwenzake kama "rafiki wa zamani." Putin pia alimtaja Xi kama "rafiki mpendwa."

Xi siku ya Jumatano alisema wizara za mambo ya nje kutoka nchi zote mbili zitahitaji kutekeleza kikamilifu makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Rais wa Urusi Vladimir Putin, akitoa wito wa kuimarisha mawasiliano ya kimkakati na uratibu wa karibu wa kidiplomasia.

Lavrov aliwasili China siku ya Jumanne kwa safari ya siku mbili kwa mwaliko wa mwenzake wa China Wang Yi.

AFP