Wolfsburg yapunguza pengo dhidi ya Bayern | Michezo | DW | 02.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Wolfsburg yapunguza pengo dhidi ya Bayern

Wolfsburg ilitamba na kuwaduwaza wenyeji Werder Bremen kwa kuwafunga mabao matano kwa matatu jana Jumapili, baada ya kujizatiti kutoka goli moja nyuma mara tatu na kufunga mabao matatu katika kipindi cha dakika tano

Matokeo hayo yaliiwezesha Wolfsburg kupunguza pengo kati yao na viongozi Bayern Munich hadi pointi nane. Daniel Caligiuri aliifungia Wolfsburg magoli mawili. "Tulikuwa nyuma magoli matatu kwa mawili katika kipindi cha mapumziko, lakini kocha alituambia kuwa nafasi zetu zitakuja na tuendelee kucheza mchezo wetu kwa sababu bado tulikuwa na dakika 45. Na bila shaka hivyo ndio mambo yalikuwa katika hatua hiyo na ushindi ukapatikana katika kipindi cha pili".

Ushindi huo ni wa sita katika mechi saba, na umewaweka Wolfsburg katika nafasi ya pili na pointi 50. Bayern wana points 58 baada ya kuwararua Cologne magoli manne kwa moja.

Bundesliga Borussia Dortmund FC Schalke 04 Ilkay Gündogan

Dortmund wanaendelea kufufuka baada ya matatizo mengi

Borussia Moenchengladbach wako katika nafasi ya tatu nyuma ya Wolfsburg na pengo la pointi 10 baada ya kuwagwangura Paderborn mabao mawili kwa sifuri matokeo ambayo yalimwacha kocha wa Gladbach Lucien Favre akiwa na tabasamu tele. "Kwa maoni yangu tulistahili ushindi huo. Kwa sababu tuliumiliki mpira na kushambulia zaidi. Tulikuwa na nafasi nyingi. Tulicheza vyema lakini bahati mbaya tulifunga mabao machache tu. Tulishindwa kuwa wabunifu mbele ya lango mchuano wote hadi tukapata ushindi wa mbili bila na hilo ndio jambo muhimu".

Siku ya Jumamosi, mshambuliaji wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang ndiye aliyekuwa shujaa wa Borussia Dortmund' alipofungua ukurasa wa magoli katika ushindi wao wa mabao matatu kwa bila dhidi ya Schalke katika mchuano mkali wa watani wa jadi wa jimbo la Ruhr.

BVB sasa wako katika nafasi ya kumi ikiwa ni ushindi wao wa nne mfululizo katika ligi, baada ya kuanza mwezi wa Februari wakishika mkia kwenye msimamo wa ligi. Jurgen Klopp ni kocha wa BVB "Hicho ndicho nilichotaka nilipoamka leo asubuhi: kuwa siku ikamilike wakati tukisimama pamoja kama watu waliopitia mambo mengi msimu huu, japokuwa bado hatujafanikiwa chochote, lakini wachezaji wangu wamezawadiwa na ushindi wa watani wa jadi na pia kwa kucheza vyema. Nina furaha hasa kwa sababu ushindi huu ni muhimu kwetu".

Kichapo hicho kimeiacha Schalke katika nafasi ya tano. Bayer Leverkusen ilisonga hadi nafasi ya nne baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Freiburg. Augsburg ilianguka katika nafasi ya sita baada ya kuzabwa bao moja kwa sifuri na Hertha Berlin.

Stuttgart inashikilia mkia baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na Hanover wakati Hoffenheim wakipata ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Mainz. Hamburg imesonga katika eneo la kushushwa daraja baada ya kurambishwa mabao mawili kwa moja na Eintracht Frankfurt.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com