Wolfsburg, Gladbach zaangazia soka la Ulaya | Michezo | DW | 16.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Wolfsburg, Gladbach zaangazia soka la Ulaya

Timu za Wolfsburg na Borussia Moenchengladbach zimeimarisha matumaini yao ya kucheza katika Ligi ya Mabingwa kufuatia ushindi wa mechi zao mwishoni mwa juma.

Kevin de Bruyne aliiongoza Wolfsburg kupata ushindi wa mabao matatu kwa bila dhidi ya Freiburg wakati Gladbach ilitegemea magoli ya Patrick Hermann kuiadhibu Hanover mbili bila.

Nambari mbili kwenye ligi Wolfsburg wako nyuma ya viongozi wa Bayern Munich na pengo la pointi 11 lakini wako mbele ya nambari nne Bayer Leverkusen katika nafasi ya mechi za mchujo za Champions League na pengo kama hilo.

Freiburg inabakia katika nafasi ya 17 na katika eneo la kushushwa ngazi baada ya kupata pointi moja tu kutokana na mechi zao nne za ligi. Oliver Sorg ni mchezaji wa Freiburg. "Nnaweza kusema hatukustahili kuchapwa tatu bila. Tulifungwa bao la upuzi katika kipindi cha kwanza kutokana na makosa ya mchezaji na hilo hutokea katika mpira. Kisha ukiwa nyuma goli moja kwa sifuri dhidi ya Wolfsburg inakuwa kazi ngumu. Na tulijaribu kucheza ili kusawazisha lakini Wolfsburg wakatuzidi nguvu na katika hali ya kutafuta goli tukaangamizwa"

Bundesliga Gladbach vs Hannover

Gladbach wanatafuta tikiti ya moja kwa moja ya kucheza Ligi ya Mabingwa - (Champions League)

Gladbach iliiruka Leverkusen ili kunyakua nafasi ya tatu na faida ya pointi mbili, ambayo ni nafasi ya mwisho ya kufuzu katika Ligi ya Mabingwa. Hivyo wako nyuma ya Wolfsburg na pengo la point inane. Huyu hapa mfungaji wa magoli ya Gladbach Patrick Hermann "Tumecheza leo mchezo mzuri sana na kushambulia kwelikweli katika kipindi cha kwanza ambapo mlinzani hangeweza kucheza kutoka katikati mwa uwanja. Mbili bila ni matokeo mazuri. Tulikuwa na nafasi nyingi siyo kwangu tu. Tumefunga mabao mawili na kuendeleza ushindi wetu."

Kwingineko, Eintracht Frankfurt walijiimarisha katika upande wa juu wa msimamo wa ligi kufuatia ushindi wa mabao manne kwa sifuri dhidi ya nambari tatu kutoka nyuma Paderborn. Mainz walipata ushindi muhimu wa mbili bila dhidi ya Augsburg, wakati Hertha Berlin wakikosa nafasi ya kunyakua pointi tatu muhimu kufuatia bao la kusawazisha la dakika ya mwisho la Joel Matip wa Schalke. Mechi hiyo iliishikamilika mbili mbili.

Hoffenheim waliyaimarisha matumaini ya kucheza Ulaya msimu ujao kufuatia ushindi wa tatu bila dhidi ya Hamburg. Borussia Dortmund ilikwama baada ya kutekwa sare ya sifuri kwa sifuri na Cologne. Bayer Leverkusen waliwararua Stuttgart nne bila.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com