Wizara ya nje ya Ujerumani ilichangia katika maovu yaliyofanywa na wanazi wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wizara ya nje ya Ujerumani ilichangia katika maovu yaliyofanywa na wanazi wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani inakabidhiwa ripoti ya kurtasa 900 iliyochunguza mchango uliofanywa na wizara hiyo katika kuandamwa mayahudi na wapinzani wa utawala wa wanazi

Wizara ya mambo ya nchi za nje mjini Berlin

Wizara ya mambo ya nchi za nje mjini Berlin

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani ilihusika sana na mauwaji ya halaiki ya wayahudi katika vita vikuu vya pili vya dunia-Holocaust. Mkuu wa kamisheni ya wanahistoria, Eckart Conze, ameilinganisha wizara ya mambo ya nchi za nje ya wakati ule na "shirika la kihalifu " lililochangia wakati ule katika visa vya uhalifu vya Wanazi. Zaidi ya hayo, baada ya mwaka 1945 wizara hiyo ilifanya kila la kufanya kuficha maovu yaliyotendeka. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti hiyo itakayokabidhiwa rasmi wizara ya mambo ya nchi za nje hii leo mjini Berlin.

Mtaalam wa historia kutoka Marburg, Eckart Conze, hakutafuna maneno alipokuwa akichambua yale yaliyotokea zamani katika wizara ya mambo ya nchi za nje. Wizara hiyo iliyokuwa katika mtaa wa Wilhelmstrasse mjini Berlin wakati wa utawala wa Wanazi, haijawa, kama inavyojinata, ngome ya wapinzani. Kinyume kabisa. Wengi wa wanadiplomasia walihisi kutwaa madaraka Hitler mwaka 1933 ni sawa na uokovu kwao-anasema Conze. Baadae wizara hiyo ikachangia katika maovu ya Wanazi. Wanadiplomasia walihusika,wachache tuu ndio waliovumilia shinikizo au kupinga,anasema mtaalam huyo wa historia, Eckart Conze:

"Wizara ya mambo ya nje ilichangia kuanzia mwaka 1933 katika sera za matumizi ya nguvu za Wanazi. Imechangia sana katika kuandamwa na baadae kuuliwa wayahudi wa Ulaya na kwa namna hiyo, na hapa mtu hawezi kusema vyengine, iligeuka pia kua shirika la wahalifu."

Miongoni mwa waliochangia kwa mfano ni pamoja na mwanadiplomasia mashuhuri ambae baadae alichaguliwa kuwa katibu wa dola, Ernst von Weizäcker, baba yake rais wa zamani wa shirikisho, Richard von Weizäcker. Alipokwenda Uswisi, akiwa mjumbe wa serikali, alifanya kila la kufanya ili mwandishi vitabu wa kijerumani, Thomas Mann, apokonywe uraia wake kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya Wanazi. Von Weizäcker alikuwa miongoni mwa wanadiplomasia wachache mashuhuri wa Ujerumani aliyehukumiwa kifungo cha miaka saba jela kutokana na kuhusika kwake na siasa za Wanazi.

Baada ya vita vikuu, wizara ya mambo ya nchi za nje ilifanikiwa kuficha mambo na zaidi ya hayo, ilifanikiwa hata kuwaonya na kuwalinda wahalifu wa vita waliokuwa wakisakwa-imetajwa katika ripoti hiyo ya kurasa 900 iliyoandikwa na wataalamu wanne wa historia.

Kwa muda wa miaka minne Eckarz Conze na mwenzake, Norbert Frei, wakishirikiana na mtaalam wa historia kutoka Marekani, Peters Hayes, na Moshe Zimmermann wa kutoka Israel walichunguza yaliyofanyika katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ujerumani wakati wa utawala wa wanazi.

Waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle ameisifu ripoti hiyo ya wataalam wa historia.Akizungumza na kituo cha televisheni cha ARD,waziri wa mambo ya nchi za nje wa serikali kuu ya Ujerumani Guido Westerwelle ameitaja kuwa "waraka muhimu" ambao unabidi kutumiwa siku za mbele kama sehemu ya mafunzo kwa wanaosomea diplomasia.

Westerwelle ameirithi tu ripoti hiyo.Alikuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa kutoka chama cha walinzi wa mazingira die Grüne,Joschka Fischer alieamuru uchunguzi huo ufanywe mnamo mwaka 2005,kufuatia mvutano uliozuka katika wizara hiyo wakati ule kuhusu kumbukumbu za wanadiplomasia waliofariki dunia.

Mwandishi:Marx,Bettina/Hamidou Oummilkheir/ZR

Mpitiaji:Miraji Othman

 • Tarehe 26.10.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PoCp
 • Tarehe 26.10.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PoCp
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com