1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa kuzuia jaribio la bomu la kinuklia

P.Martin6 Oktoba 2006

Madola makuu hii leo yanatazamiwa kuidhinisha hati inayotoa wito kwa Korea ya Kaskazini,kuachilia mbali mpango wa kutaka kujaribu bomu lake la kinuklia.

https://p.dw.com/p/CHLJ
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: AP

Hati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa isiyotoa wazi wazi kitisho cha vikwazo, haitazamiwi kuwa na maneno makali,kinyume na mapendekezo ya Marekani na Japan.Wakati ambapo Marekani na Korea ya Kusini zinasema haziwezi kustahmilia Korea ya Kaskazini yenye silaha za kinuklia,Japan imetoa wito wa kuwekwa vikwazo, vikiwemo vikwazo vya silaha,biashara na uchumi kuambatana na kipengele cha saba cha katiba ya Umoja wa Mataifa.

Kwa upande mwingine,China ilio mshirika mkuu wa Korea ya Kaskazini,imeitaka Pyongyang iwe na uvumilivu.Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Urussi,Sergei Lavrov amesema,Urussi imezungumza moja kwa moja na serikali ya Pyongyang.China na Urussi zinajulikana kuwa zinapinga kuiwekea Pyongyang vikwazo vikali.

Hati ya hivi sasa itaihimiza Korea ya Kaskazini kutofanya jaribio la silaha yake ya kinuklia na ijiepushe na hatua yo yote ile ambayo itaweza kuzidisha mvutano.Hati hiyo pia itatoa mwito kwa Pyongyang kurejea moja kwa moja katika majadiliano ya pande sita,bila ya kutoa masharti. Vile vile kwa haraka,itekeleze ahadi iliyotolewa Septemba mwaka 2005 kuwa itaachilia mbali mradi wake wa kinuklia pindi itanufaika katika sekta ya nishati na usalama. Kufuatia juhudi za Marekani kutaka kukata mawasiliano ya Korea ya Kaskazini katika mfumo wa mabenki ya kimataifa,serikali Pyongyang,tangu mwezi wa Novemba imesusa kushiriki katika majadiliano pamoja na China, Japan,Korea ya Kusini,Urussi na Marekani.Kwa mujibu wa gazeti la Chosun Sinbo linalochapishwa na Wakorea nchini Japan na linalodhaniwa kuwakilisha maoni ya Pyongyang,jaribio la kinuklia haliwezi kuepukwa,ikiwa Marekani haitokuwa na msimamo wa usuluhishi kuhusu majadiliano hayo.Vyombo vya habari vya Kijapani vimesema kuwa siku ya Jumatano,ndege ya jeshi la Kimarekani,yenye uwezo wa kuchunguza majeribio ya kinuklia iliruka kutoka kituo cha jeshi la anga la Marekani kilicho Okinawa nchini Japan na ndege hiyo ilielekea Ras ya Korea,lakini wizara ya ulinzi ya Marekani imekataa kuthibitisha au kukanusha ripoti hiyo.

Kwa upande mwingine,waziri wa mambo ya kigeni wa Korea ya Kusini,Ban Ki-Moon anaetazamiwa kuwa kiongozi mpya wa Umoja wa Mataifa,amesema yeye yupo tayari kwenda Pyongyang kwa majadiliano ya kutafuta njia ya kusitisha mradi wa kinuklia wa Korea ya Kaskazini.