Wimbi la wizi wa mifugo lazusha Mauaji ya Kikabila nchini Kenya | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wimbi la wizi wa mifugo lazusha Mauaji ya Kikabila nchini Kenya

Kuzuka kwa wimbi la wizi wa Mifugo nchini Kenya kumezusha uadui wa kikabila katika eneo la bonde la ufa na kusababisha mauaji ya watu ishirini na tano.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya kushoto na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, katikati na kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga, kulia mjini Nairobi.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya kushoto na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, katikati na kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga, kulia mjini Nairobi.

Raia wa Kenya aliyekuwa akituhumiwa kuandaa mpango wa kufanyika kwa machafuko ya kikabila katika uchaguzi uliopita amekanusha na kuishutumu Serikali kuwa inatafuta njia za kuitupia lawama jamii ya kabila la Kalenjin nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi nchini Kenya, Joseph Ashimalla, katika vurugu zilizotokea jana, wanakijiji kumi na mbili waliuawa na wezi hao wa mifugo katika Wilaya ya Baringo.

Kufuatia vurugu hizo Polisi waliamua kuingilia kati ili kutuliza hali hiyo ambapo wezi wa mifugo watano waliuawa katika kufyatuliana risasi kulikofutia baada ya kuona vurugu zinazidi kuendelea.

Kamanda Ashimalla, amesema shambulio hilo limesababisha kuongeza idadi ya watu waliouawa na kufikia ishirini na tano katika siku za hivi karibuni kwenye matukio ya wezi wa mifugo ambayo yamesababisha kuwepo kwa uadui baina ya makabila ya Turkana, Samburu na katika jamii ya wapokot kwenye eneo hilo.

Mauaji hayo siyo tu kwamba yanahusishwa na vurugu zilizofuatia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Desemba mwaka jana nchini humo bali pia yamekuwa yakionekana kama ni sehemu ya mapigano yaliyo sababishwa na vurugu za Kisiasa.

Juzi jumanne, Wabunge waliunga mkono kushirikiana katika kugawana madaraka katika ngazi ya Serikali, ikiwa ni juhudi za kumaliza mzozo wa Kisiasa nchini humo, hata hivyo wameonya kwamba kunahaja ya kuyaangalia zaidi mapigano haya ya kikabila na ya Ardhi.

Aidha Msemaji wa Polisi nchini humo, Eric Kiraithe amesema Serikali itafanya kila jitihada ili kuhakikisha mapigano hayo yanakomeshwa na kuhakikisha sheria na utulivu vinarejeshwa katika maeneo hayo yaliyoathirika na machafuko hayo.

Erick Kiraithe, ametangaza pia kushitakiwa kwa watu watano ambao wanahusishwa na kuchoma moto mali za watu kwa makusudi wakati wa vurugu za uchaguzi karibu na mji wa Eldoret na ikiwa watakutwa na hatia hiyo, basi watakabiliwa na kifungo cha maisha.

Hata hivyo polisi bado wanaendelea kumtafuta Mkuu wa kundi la waasi la wasabaoti aliyeko mafichoni anayetuhumiwa kuandaa vurugu zilizotokea kaskazini Magharibi mwa eneo la mlima elgon.

Katika kipindi cha muda mrefu, eneo la Mlima Elgon limekuwa na machafuko ambako mamia ya watu wameshauawa na wengine sitini na sita wamelazimika kuyahama makazi yao tangu kuzuka kwa machafuko ya damu Desema mwaka 2006.

Wakati huo huo mzee mmoja raia wa Kenya ambaye pia anashutumiwa kuandaa mpango wa kufanyika machafuko ya kikabila katika uchaguzi uliopita amekanusha na kuishutumu Serikali kuwa inatafuta njia za kuitupia lawama jamii ya kabila la Kalenjin nchini humo.

Jackson Kibor mwenye umri wa miaka sabini na tatu na mwenyekiti wa Wazee wa chama cha upinzani cha ODM katika eneo la bonde la ufa nchini Kenya, amenukuliwa akisema kwamba yeye ni mzee na umri wake haumruhusu kuingia vitani.

Amesema polisi walimsingizia kuhusika katika kulichoma moto Kanisa katika mji wa Kiambaa lakini ukweli ni kwamba yeye hakuwepo katika eneo hilo na wala hafahamu eneo hilo liko upande gani lakini anachokijua mauaji hayo yalikuwa ni yakutisha yaliyofanywa na kundi la watu wenye hasira.

Tayari Rais Kibaki na chama cha upinzani cha ODM wameshakubaliana kugawana madaraka ili kumaliza mapigano.

Makundi ya haki za binadamu yanaishinikiza Serikali ya nchi hiyo kuwatafuta na iwakamate wale wote waliyonyuma ya mashambulizi hayo makubwa ambayo hayajawahi kutokea tangia Taifa hilo la Afrika Mashariki lipate uhuru wake mwaka 1963.

 • Tarehe 20.03.2008
 • Mwandishi Scholastica Mazula
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DRtV
 • Tarehe 20.03.2008
 • Mwandishi Scholastica Mazula
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DRtV
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com