1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto asema kesi imefutiliwa kwa sababu hawakuwa na hatia.

John Juma8 Aprili 2016

Ruto amekataa kauli ya mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kibinadamu kuwa kesi hiyo imefutiliwa mbali kwa sababu ya muingilio wa kisiasa na vitisho kwa mashahidi, bali anasisitiza ni kwa sababu hawana hatia.

https://p.dw.com/p/1IRtP
Naibu rais wa Kenya William Ruto
Naibu rais wa Kenya William RutoPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Naibu wa rais wa Kenya William Ruto kwa mara ya kwanza amezungumzia kutupiliwa mbali kwa kesi iliyomkabili katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kibinadamu-ICC mjini The Hague.

Kwenye hotuba yake kwa wanahabari katika makazi yake jijini Nairobi, William Ruto amesema kutupiliwa kwa kesi hiyo ni ishara kuwa hakuwa na hatia. Ameongeza kuwa amewasamehea wale wote waliopanga njama ya kesi hiyo dhidi yake.

Amesisitiza kuwa atashirikiana na rais Uhuru Kenyatta na serikali kwa jumla kuhakikisha wanapatanisha taifa zima na kuleta Wakenya wote pamoja na serikali itahakikisha walioathiriwa wote wanashughulikiwa ipasavyo.

Muingilio wa kisiasa

William Ruto amesema kesi iliyomkabili katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kibinadamu ICC, pamoja na mtangazaji Joshua Arap Sang', ilitupiliwa mbali kwa sababu hawakuwa na hatia.

Majaji wa mahakama hiyo nchini The Hague walitupilia mbali kesi hiyo wakisema muingilio wa kisiasa kwenye kesi hiyo umeifanya kukosa kuendelea vyema.

Kwenye hotuba yake ya kwanza kuhusu uamuzi wa kesi hiyo uliotolewa mapema wiki hii, William Ruto amesema hakushiriki katika kununua silaha wala kupanga umwagikaji wa damu uliotokea baada ya uchaguzi wa Disemba mwaka 2007 ambao ulizua utata na kusababisha kuuawa kwa watu 1,200.

“Madai yaliyowekwa dhidi yangu yalikuwa uhalifu uliopangwa, njama potovu za uongo dhidi yangu,” alisema Ruto.

Machafuko Kenya baada ya uchaguzi 2007
Machafuko Kenya baada ya uchaguzi 2007Picha: picture-alliance/AP Photo

Msamaha kwa waliopanga njama

Amesisitiza kuwa atashirikiana na rais Uhuru Kenyatta na serikali kwa jumla kuhakikisha wanapatanisha taifa zima na kuleta wakenya wote pamoja. Kadhalika amekariri kuwa serikali ya Kenya itahakikisha imewashughulikia kikamilifu waathiriwa wote wa machafuko hayo ya kisiasa.

Akiandamana na familia yake akiwemo mama yake mzazi na mkewe, Ruto anayetarajiwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 alikataa kauli ya mahakama ya ICC kuwa kesi hiyo ilitupiliwa mbali kwa sababu ya muingilio wa kisiasa na vitisho dhidi ya mashahidi.

Kesi sawa na hiyo katika mahakama ya ICC dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta pia ilifutiliwa mbali mwaka jana kufuatia kutoweka kwa ushahidi uliotolewa na mashahidi.

Katika kesi zote mbili, upande wa mashtaka wamedai mashahidi walihongwa au kutishwa kuondoa ushahidi waliotoa awali.

Mwandishi: John Juma/RTRE

Mhariri:Iddi Ssessanga