Wikiendi ya chaguzi Afrika | Matukio ya Afrika | DW | 18.03.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Wikiendi ya chaguzi Afrika

Jumapili Machi 20 ni siku ya chaguzi kadhaa barani Afrika- nchi nne za Afrika magharibi na moja Afrika kati. Nchi hizo ni Benin, Niger, Cape verde, Senegal na Jamhuri ya Congo .

Zinsou kushoto na mpinzani wake Talon

Zinsou kushoto na mpinzani wake Talon

Nchini Benin ni duru ya pili ya uchaguzi wa rais, washindani wakiwa Waziri mkuu lionel Zinsou na Mfanyabiashara Patrice Talon waliomaliza nafasi ya kwanza na ya pili katika duru ya kwanza Machi 6. Talon anaungwa mkono na mgombea mwengine Sebastien Ajon aliyemaliza nafasi ya tatu na kushindwa kuingia duru ya pili. Mshindi atachukua nafasi itakayoachwa na rais wa sasa Thomas Boni Yayi ambaye anamaliza muhula wake wa pili , wa mwisho kwa mujibu wa katiba. Benin inatajwa kuwa ni mfano wa kuigwa panapohusika na ustawi kwa demokrasia barani Afrika na kuheshimiwa uamuzi wa raia .

Kibarua kigumu kwa wapinzani:

Duru ya pili ya uchaguzi wa rais na bunge inafanyika pia Niger. Rais Mahamadou Issoufou anachuana na kiongozi wa upinzani Hama Amadou, aliyemaliza wa pili katika duru ya kwanza mwezi uliopita ambayo ilishindwa kumpata mshindi wa moja kwa moja aliyevuka asilimia 50 ya kura. Amadou ambaye ni spika wa zamani wa bunge, alishuhudia duru hiyo ikifanyika akiwa gerezani akikabiliwa na kashfa ya biashara ya watoto wadogo wanaouzwa kwa matajiri wasio na watoto. Binafsi amekanusha madai hayo akisema yana malengo ya kisiasa.

Mgombea Hama Amadou

Mgombea Hama Amadou

Wapinzani wa rais Issoufou wanadai kuwa kiongozi huyo ameanza kuwa na muelekeo wa kidikteta. Amadou mwenye umri wa miaka 66 alitolewa gerezani siku chache zilizopita na kupelekwa Ufaransa kwa mataibabu baada ya afya yake kuwa mbaya. Hali yake sasa inasemekana kuendelea vizuri.

Mfano mzuri wa kuigwa :

Visiwa vidogo katika kanda hiyo ya Afrika magharibi Cape Verde kesho vinauchaguzi wa bunge.washindani wakuu ni vyama vitatu- Chama tawala -PAICV,Chama cha MPD) UCID. Cape Verde iliojinyakulia uhuru kutoka kwa Ureno 1975 inasifika pia kwa utekelezaji wa demokrasia na hata kubadiloishana utawala kati ya washindi na washindwa bila ya mizengwe.

Rais Macky Sall

Rais Macky Sall

Huko Senegal inaitishwa kura ya maoni hapo kesho kuhusu kubadili kifungu cha katiba kuhusu kipindi cha kuhudumu kama rais, kutoka mihula miwili ya miaka saba kila moja na kurejeshwa utaratibu wa zamani wa miaka mitano, kwa kila mhula mmoja, huku n ukiwepo mfumo ule ule wa mihula miwili pekee. Mwaka jana Rais Macky Sall anayeunga mkono mabadiliko hayo, amesema pindi mabadiliko hayo yakipitishwa yataanza kutumika baada ya kipindi chake cha sasa kumalizika 2019. Mengine yanayopendekezwa katika kura ya maoni ni mabadiliko ya sheria za uchaguzi na kulipa madaraka zaidi bunge la taifa na baraza la katiba.

Kiongozi wa muda mrefu Sassou Nguesso

Kiongozi wa muda mrefu Sassou Nguesso

Jee Nguesso atabakia madarakani ?

Mbali na Afrika magharibi katika Jamhuri ya Congo,au Congo Brazzaville katika ukanda ya Afrika kati , wapiga kura watakuwa vituoni pia baada ya rais Denis Sassou Nguesso kubadili katiba ili aweze kuendelea. Kiongozi huyo wa muda mrefu akiwa na azma ya kuendelea kubakia madarakani aliitisha kura ya maoni hapo kabla iliosusiwa na baadhi ya wapinzani na kubadiloi kifungu cha katiba kiliochokuwa kikimzuwiakugombea kwa sababu ya umri na muda aliokwishatumika katika wadhifa huo. Mpinzani wake mkuu ni mkuu wa zamani wa majeshi Jenerali Jean-Marie Michel Mokoko aliyekuwa hadi hivi karibuni mshauri wa rais Nguesso kabla ya kujiuzulu na kutangaza kuwa atagombea urais dhidi ya bosi wake wa zamani. Kinachosubiriwa kuonekana ni ikiwa wakongo Brazzabille wataamua kuwa na mbadala au kuendelea na Nguesso.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, rtr, afp,ap

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com