1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yazionya nchi kutoweka marufuku ya jumla ya kusafiri

Bruce Amani
1 Desemba 2021

Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO limezionya nchi kutoweka marufuku ya jumla ya kusafiri kutokana na kirusi kipya cha Omicron. Wanasayansi wanajaribu kubaini ni kiasi gani cha kinga ambacho chanjo za sasa zinaweza kutoa

https://p.dw.com/p/43gMZ
USA Symbolbild Flugzeug
Picha: Steve Parsons/PA Wire/empics/picture alliance

Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO limezionya nchi kutoweka marufuku ya jumla ya kusafiri kutokana na kirusi kipya cha Omicron. Serikali mbalimbali na wanasayansi wanajaribu kubaini ni kiasi gani cha kinga ambacho chanjo za sasa zinaweza kutoa dhidi ya kirusi hicho.

Soma pia:WHO: Huenda kirusi cha Omicron kikasambaa kote duniani

WHO imezitaka nchi kutumia mbinu ya ushahidi na athari zilizopo wakati wa kutangaza hatua zozote za kusafiri, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuwachunguza au kuwaweka karantini abiria wa kimataifa. Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema anafahamu kuna wasiwasi kuhusu Omicron, lakini marufuku ya jumla ya kusafiri haitokizuia kirusi hicho kusambaa.

Olaf Scholz
Olaf Scholz anataka chanjo ya lazima itolewe kwa ummaPicha: Clemens Bilan/Getty Images

Kampuni ya BioNTech imeelezea matumaini kuwa chanjo inayotengeneza kwa ushirikiano na Pfizer inaweza ikatoa kinga imara dhidi ya Omicron. Visa vya kirusi hicho kipya vimesambaa, huku kisa cha kwanza kikiripotiwa Amerika Kusini nchini Brazil.

Soma pia:Kirusi cha Omicron chazusha taharuki ulimwenguni

Nchini Ujerumani kansela mtarajiwa Olaf Scholz amesema ataunga mkono pendekezo la kutoa chanjo ya lazima kwa kila mtu mwaka ujao, lakini wabunge watakuwa huru kupiga kura kulingana na hisia zao kuhusu suala hilo. 

Wanasiasa Ujerumani sasa wanataka kuwekwe masharti makali zaidi ya kudhibiti virusi vya corona baada ya kiwango cha maambukizi cha siku saba nchini humu kuvunja rekodi. 

Msemaji wa masuala ya afya wa chama cha Kijani Janosch Dahmen ameliambia shirika la habari la dpa kwamba kuna haja ya uchumi kufungwa kwa muda katika baadhi ya majimbo ili kulivunja wimbi la nne la maambukizi.

Tamko lake linakuja wakati ambapo kumekuwa na maandamano kaskazini mashariki mwa Ujerumani huku waandamanaji wakipinga vikwazo vipya vinavyowekwa kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Wakati huo huo Mahakama Kuu ya Kikatiba nchini Ujerumani imetoa hukumu yake ya kwanza ambapo imesema uamuzi wa kuzuia shughuli za maisha na uhuru wa watu katika kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona ulikuwa halali.

AFP, Reuters, DPA, AP