1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Hatukubaliani na mtazamo wa Magufuli

7 Mei 2020

Shirika la Afya Duniani WHO limekanusha madai ya Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania kwamba vipimo vya virusi vya corona vina hitilafu.

https://p.dw.com/p/3buYE
WHO - Ebola-Lage im Kongo | Matshidiso Moeti
Picha: picture-alliance/dpa/KEYSTONE/S. Di Nolfi

Katika mkutano na waandishi wa habari, mkurugenzi wa WHO barani Afrika Matshidiso Moeti amesema "tuna uhakika kwamba hakukuwepo na virusi hivyo awali katika vipimo, hatukubaliani na mtazamo wa Magufuli."

Kauli hii ya WHO imekuja baada ya Rais Magufuli Jumapili iliyopita kusema kwamba vipimo hivyo vina hitilafu baada ya kuonyesha maambukizi ya corona katika majimaji ya tunda la papai na mbuzi. Tanzania ina jumla ya visa 480 vya maambukizi ya corona ingawa wizara ya afya nchini humo haijatoa taarifa mpya kwa kipindi cha juma moja sasa.

Waliofariki Zanzibar 32 baada ya mtu mmoja kufariki Alhamis

Huku hayo yakiarifiwa, Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kupitia wizara yake ya afya imethibitisha visa vinane vya virusi vya corona na kufikisha idadi jumla ya maambukizi kisiwani humo kufikia 235. Wizara hiyo imesema watano kati yao wanaishi Unguja na watatu huko Pemba.

Tanzania President John Pombe Magufuli in Dar es Salaam
Rais wa Tanzania John Pombe MagufuliPicha: DW/S. Khamis

Mtu mmoja amefariki na kufikisha idadi ya walioaga dunia kutokana na virusi hivyo kisiwani Zanzibar kufikia watu 32.

Haya yanajiri wakati ambapo idadi ya waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 kote duniani imeongezeka na kufikia zaidi ya watu 263,000 huku watu milioni 3.7 wakiwa wameambukizwa.

Barani Ulaya, visa vya maambukizi ya virusi vya corona Urusi vimepanda katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita na sasa nchi hiyo imeipiku Ufaransa na Ujerumani na kushikilia nafasi ya tano katika nchi zenye maambukizi mengi zaidi duniani. Fauka ya hayo meya wa mji wa Moscow amesema, idadi kamili ambayo haijajumuishwa kwenye takwimu, iko juu zaidi.

Idadi kamili ya walioambukizwa imeongezeka na kufikia watu 177,160 huko Urusi baada ya visa vya maambukizi mapya kuongezeka kwa 11,231 kwa siku moja tu. Zaidi ya nusu ya visa hivyo pamoja na vifo viko katika Mji Mkuu Moscow ambao ndio kitovu cha mripuko wa virusi hivyo Urusi. Moscow na maeneo mengine Urusi yako katika wiki yake ya sita ya marufuku ya kutotoka nje.

Tukisalia Ulaya, Taasisi ya Robert Koch nchini Ujerumani, imesema kwamba kiwango cha maambukizi Ujerumani kimepungua ila kimeonya kwamba huenda kukazuka wimbi la pili la maambukizi hasa katika msimu wa mapukutiko.

Ujerumani hapo jana Jumatano ililegeza zaidi vikwazo ilivyokuwa imeviweka. Bodi ya Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga DFL imetangaza kwamba mechi za ligi hiyo zitaanza tena kuchezwa mnamo Jumamosi Mei 16 huo ukiwa ni mzunguko wa ishirini na sita wa mechi za Bundesliga. Mechi hazitoanza Ijumaa kama ilivyo ada katika Bundesliga na badala yake mechi za kwanza zitakuwa Jumamosi ya kwanza ikiwa ile ya Rugr dabi kati ya Borussia Dortmund na Schalke 04. Ligi hiyo inatazamiwa kuumaliza msimu wake Juni 27.

India yaanza kuwarudisha nyumbani raia 15,000 walio nchi za nje

Kwengineko duniani China inaituhumu Marekani kwa kujaribu kuisukumizia lawama kuhusiana na virusi vya corona, baada ya Rais Donald Trump kusema kwamba janga hili ni baya kuliko lile tukio la Bandari ya Pearl au lile shambulizi la kigaidi la Septemba 2001.

USA Coronavirus Donald Trump
Rais Donald Tump wa MarekaniPicha: Reuters/C. Barria

Katika hilo shambulizi la Bandari ya Pearl, Japan iliishambulia kambi ya wanajeshi wa majini wa Marekani huko Hawaii na kuisababisha Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na hilo shambulizi la kigaidi la Septemba 2011 lilisababisha vifo vya karibu watu 3,000.

Na huko India, hatua ya kwanza ya zoezi la kuwarudisha nyumbani maelfu ya Wahindi waliokwama katika nchi za nje kutokana na virusi vya corona linaanza leo Alhamis huku ndege mbili za shirika la Emirates zikitumika katika shughuli hiyo. India iliweka marufuku ya ndege za kimataifa kuingia nchini humo mwezi Machi hivyo kuwazuia maelfu ya wafanyakazi na wanafunzi waliokuwa nje ya nchi kurudi nyumbani. Jumla ya watu 15,000 kutoka nchi 12 watasafirishwa kwa ndege na meli za kijeshi.

Nako nchini Misri, Waziri Mkuu Mostafa Madbouly ametangaza kwamba marufuku ya kutotoka nje usiku kote nchini humo yameongezwa hadi mwisho wa mwezi wa mfungo wa Ramadhani, ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.