1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ikulu ya White House yashtumiwa kwa kumtetea Trump

Tatu Karema
27 Septemba 2019

Ikulu ya White House imeshutumiwa kwa kujaribu kuficha mawasiliano ya simu kati ya rais Donald Trump ambayo anadaiwa kuishinikiza Ukraine kuingilia katika uchaguzi wa Marekani wa mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/3QL3v
USA UN-Generalversammlung Donald Trump und Wolodymyr Selenskyj
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Malalamishi hayo yanahitimisha wiki ya ufichuzi ambao umeuweka uongozi wa Trump katika hali ya kuyumba huku serikali yake, wizara ya sheria na wizara ya mambo ya nje zote zikihusika katika sakata hilo linalozidi kukithiri. Shutuma hizo zinadai kuwa maafisa wakuu wa ikulu ya Marekani wamesema kuwa huenda wamemshuhudia rais akiitumia vibaya mamlaka yake kwa manufaa binafsi katika mawasiliano hayo ya simu ya mwezi Julai na kiongozi wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Madai hayo ya uvunjaji wa sheria yanamuangazia Trump akimhimiza Zelensky kumchunguza mpinzani wake wa kisiasa nchini humo Joe Biden na kuibua malalamiko na kuchochea uchunguzi wa bunge wa kutaka kumng'oa madarakani.Mfichuaji siri huyo anayesema kuwa ameongea na takriban maafisa wakuu sita wa serikali ya Marekani, amehitimisha kuwa Trump anatumia mamlaka yake kutafuta taifa la nje kuingilia katika uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2020.

 Duell Donald Trump Impeachment eng
Kibonzo cha wito wa kung'atuliwa mamlakani kwa Trump

Kulingana na mfichuaji siri huyo, amefahamishwa na maafisa wakuu kadhaa kwamba maafisa wakuu wa ikulu ya White House wameingilia kati kuficha rekodi zote za mawasilaino hayo ya simu hasa nakala ya maneno ya mazungumzo ya simu iliyotolewa. Spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi aliongoza shutuma za chama cha Democratic dhidi ya Trump na wale wanaodaiwa kuficha nakala kamili ya maneno ya mazungumzo katika mfumo wa rekodi za kielektroniki unaoweza kufikiwa na wachache na kuwaambia wanahabari kwamba hii ni hali ya kuficha ukweli.

Spika huyo alizindua uchunguzi rasmi wa kumuondoa madarakani rais huyo siku ya Jumanne. Kufika jana, wengi wa wabunge 435, ambao 218 wa chama cha Democratic na mmoja anayejisimamia wamesema kuwa wanaunga mkono uchunguzi huo. Katika matamshi aliyotoa faragha kwa ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Trump alimshtumu afisa wa ujasusi kuwa, ''mpelelezi'' na kuyafananisha madai hayo ya mfichuzi wa siri kuwa usaliti kwa serikali.

Wabunge wa chama cha Democratic wamependekeza kuwa mashambulizi kama hayo yanavunja sheria.Huku wabunge wengi wa chama cha Republican ikiwa ni pamoja na kiongozi wa walio wachache bungeni Kevin McCarthy wakimtetea Trump na kushutumu madai ya mfichua siri huyo, wengine wanasema wanatatizika pakubwa.Katika ujumbe aliotuma kupitia mtandao wa Twitter, mbunge wa chama cha Republican Will Hurd amesema jana kuwa kuna madai mengi kutoka kwa mfichua siri huyo ambayo yanatia wasiwasi na kwamba wanahitaji kuchunguza madai yote.

Joseph Maguire, kaimu mkurugenzi wa idara ya ujasusi wa kitaifa amesisitiza kuwa hafahamu jinsia ya mfichuo siri huyo. Hapo jana Alhamisi, gazeti la New york Times liliripoti kuwa ni afisa mwanamume wa idara ya ujasusi anayehusika na ikulu ya White House.