Westerwelle aizuru China | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.10.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Westerwelle aizuru China

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle yuko ziarani nchini China kukutana na wawakilishi wa mashirika ya kiraia na wa serikali huku nchi hizo zikitangaza kuridhika na uhusiano wao wa miaka 40 sasa.

Guido Westerwelle na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Yang Jiechi.

Guido Westerwelle na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Yang Jiechi.

Tayari Westerwelle amekutana mjini Beijing na wanablogu wa mitandao kujadili maendeleo yao nchini humo. Akiwa mjini Beijing, Westewelle hakusema wazi iwapo atalizusha suala la hatima ya mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel wa mwaka 2010, Liu Xiabao, aliyeko gerezani na mke wake ambaye yuko katika kifungo cha nyumbani wakati wa mazungumzo yake na viongozi wa serikali ya China. Mwanaharakti huyo wa haki za kiraia amekuwa gerezani kwa miaka minne sasa.

Kiongozi huyo amesema haki za binaadamu, haki za kiraia na haki za mdahalo zina dhima katika uhusiano wa kidiplomasia na bila ya shaka hatima za watu binafsi.

Lakini ametaka ifahamike kwamba hayo sio mambo pekee watakayozungumzia rasmi na viongozi wa China.Ameongeza kusema kwamba pia wangelipenda kuwasaidia watu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akiwa nchini China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, akiwa nchini China.

Hapo jana nchi hizo mbili zimetangaza kwamba zimeridhika na maendeleo ya ushirikiano wao tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa nchi hizo mbili miaka 40 iliyopita. Westerwelle amezungumzia juu ya mafanikio makubwa kwa nchi zote mbili baada ya kukutana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa China, Yang Jiechi, mjini Beijing.

Yang amesema anataka nchi hizo mbili kuweka kando tafauti zao na kuendeleza kile chenye maslahi ya pamoja ili kusonga mbele na ushirikiano wao wa kimkakati.Ameongeza kusema kwamba wanataka wawe marafiki wanaoheshimiana.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa China ameahidi kwamba nchi yake itaunga mkono juhudi za kutatuwa mzozo wa madeni unaolikumba eneo linaloitumia sarafu ya euro barani Ulaya.

Ujumbe wa Ujerumani na China ukikutana mjini Peking.

Ujumbe wa Ujerumani na China ukikutana mjini Peking.

Yang pia amesema China inataraji kwamba Ujerumani itasaidia kutafuta ufumbuzi wa mzozo kuhusiana na shutuma dhidi ya kampuni za China kwamba zinauza kwa bei ya kutupwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya jua.

Westerwelle kwa upande wake ametowa wito wa kufikiwa kwa ufumbuzi wa amani mzozo wa kuwania visiwa kati ya China na Japani na mataifa mengine katika eneo la Bahari ya China Kusini na Mashariki.

"Sisi Wajerumani tunakaribisha hatua zote ambazo zinapelekea utatuzi wa masuala yaliokosa ufumbuzi kwa utulivu na makubaliano ya pande mbili." Amesema Westerwelle.

Baadae leo hii Westerwelle ataelekea Shenyang magharibi ya kaskazini mashariki ya China ambapo kampuni ya kutengeneza magari ya BMW AG ina kiwanda chake na ambapo atafunguwa ubalozi mdogo wa Ujerumani.

Hapo jana nchi hizo mbili Ujerumani na China zimesheherekea kwa tafakuri kubwa miaka 40 tokea kuanzishwa kwa uhusiano wa nchi hizo mbili.

Mwishoni mwa mwezi wa Augusti Kansela Angela Merkel na nusu ya baraza lake la mawaziri walizuru China.

Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com