Waziri wa nje wa Marekani aendelea na ziara yake barani Asia | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri wa nje wa Marekani aendelea na ziara yake barani Asia

Marekani na Japan wakubaliana wanajeshi 8000 wa Marekani wahamishiwe Guam kutoka Okinawa

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani na mwenyeji wake wa Japan

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani na mwenyeji wake wa Japan►Waziri mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton leo amezungumzia kuendeleza usawa na upatanifu katika sera ya kigeni ya Marekani, msimamo unaotofautiana na ule wa utawala wa rais wa Marekani aliyeondoka madarakani, George W Bush. Bi Clinton ameyasema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri wa kigeni wa Japan Hirofumi Nakasone mjini Tokyo Japan, kituo chake cha kwanza cha ziara yake ya siku nne barani Asia.


Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Hilary Rodham Clinton amesifu uhusiano kati ya Marekani na Japan na kuongeza kuwa nchi hizo mbili zinahitaji kushirikiana kukabiliana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaoikabili dunia. Bi Clinton ameishukuru Japan kwa ushirikiano wake katika operesheni dhidi ya ugaidi nchini Afghanistan iliyojulikana kama Operation Enduring Freedom na vile vile kusaidia kupambana na uharamia katika pwani ya Somalia.


"Pia ningependa kuishukuru Japan na Wajapani wote kwa msaada wenu katika operesheni ya Enduring Freedom. Umekuwa muhimu sana kwa ufanisi wa jeshi la muungano nchini Afghanistan. Pia naishukuru Japan kwa kutuma meli mbili za kijeshi katika ghuba ya Aden kusaidia kupambana na tatizo la uharamia."


Waziri Hilary Clinton kwa niaba ya rais wa Marekani Barack Obama, amemualika waziri mkuu wa Japan Taro Aso kwenda Washington juma lijalo. Taro Aso atakuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kumtembelea rais Obama katika ikulu ya white house Februari 24.


Kuhusu Korea Kaskazini, Bi Hillary Clinton, amerudia pendekezo la Marekani kurejesha uhusiano wa kawaida na kusaini mkataba wa amani na nchi hiyo iwapo itaangamiza mpango wake wa nyuklia. Amesema jaribio la kombora la masafa marefu inalotaka kulifanya Korea Kaskazini halitaisidia kuendeleza uhusiano wake na Marekani.


"Tunafahamu kazi inayotusubiri si rahisi. Tutachunguza tulipofikia leo na kutathmini njia muafaka ya kuchukua hivi sasa. Lengo letu linabaki lile lile; Korea Kaskazini isiyo na silaha za nyuklia. Jaribio la kombora ambalo Korea Kaskazii inalizungumzia halitasaidia kamwe kuendeleza ushirikiano wetu mbele."


Hapo kabla Bi Clinton alitia saini mkataba pamoja na waziri wa kigeni wa Japan Hirofumi Nakasone, kuwahamisha wanajeshi takriban 8,000 kati ya wanajeshi 13,000 wa Marekani walio katika kisiwa cha Okinawa kwenda eneo la Guam lililo himaya ya Marekani katika eneo la Pacific.


"Tumesaini mkataba wa kimataifa wa Gwam kwa niaba ya mataifa yetu. Mkataba huu unaongezea nguvu msingi wa ulinzi wa Japan dhidi ya mashambulio kwa njia yoyote ile. Unaelez michango ya pamoja ya nchi zetu katika kuwahamisha wanajeshi wetu kutoka kisiwa cha Okinawa hadi eneo la Gwam."


Kuendelea kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani katika kisiwa cha Okinawa kumekuwa chanzo kikubwa cha mivutano katika uhusiano baina ya Marekani na Japan.


Bi Clinton amezitembelea familia za Wajapani waliotekwa nyara na Korea Kaskazini katika miaka 1970. Amesema Marekani itafanya kila iwezalo kuishinikiza Korea Kaskazini kuwaachia huru mateka hao.


Hillary Clinton ameanza siku yake kamili ya kwanza barani Asia kwa kulitembelea eneo takatifu la Meiji mjini Tokyo, ambako alishiriki kwenye ibada ya utakaso kwenye madhabahu ya Shinto, yaliyojengwa kwa heshima ya mfalme Meiji, anayechukuliwa kuwa baba wa taifa la kisasa la Japan. Clinton ataondoka Japan kwenda Indonesia, kituo chake cha pili cha ziara yake ya Asia.


Sambamba na hayo waziri wa fedha wa Japan Shoichi Nakagawa ametangaza leo atajiuzulu kufuatia kisa cha kutia aibu wakati wa mkutano na waandishi habari mjini Roma Italia wiki iliyopita. Kiongozi huyo alionekana mlevi huku akiyafunga macho yake wakati alipoyajibu maswali ya waandishi wa habari yaliyoelekezwa kwa gavana wa benki ya Japan, Masaaki Shirakawa, aliyekuwa amekaa kando yake.

 • Tarehe 17.02.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gvs5
 • Tarehe 17.02.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gvs5
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com