Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice kufanya ziara ya kihistoria Libya | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice kufanya ziara ya kihistoria Libya

Ziara ya kihistoria ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice nchini Libya wiki hiii inaanzisha enzi mpya ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuweka kando miongo kadhaa ya uhasama na kutengwa kwa Libya.

Condoleezza Rice waziri wa mambo ya nje wa Marekani.

Condoleezza Rice waziri wa mambo ya nje wa Marekani.

Ziara ya Rice ni ya kwanza kufanywa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani kwa Libya tokea mwaka 1953 na inafanyika ikiwa ni miaka mitano baada ya Libya kutangaza kwamba inaachana na mpango wake wa kutengeneza silaha za maangamizi makubwa.

Uhusiano wa Marekani na Libya ulianza kuwa mzuri hapo mwaka 2003 wakati kiogozi wa Libya Muammar Gaddafi alipokubali kuachana na mipango ya kutengeneza silaha za maangamizi makubwa na kuukana ugaidi.

Kutoka na uamuzi wake huo Marekani ikakomesha uwekaji wa vikwazo dhidi ya nchi hiyo,ikaiondowa nchi hiyo kwenye orodha yake mbaya ya ugaidi na ikaanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia.Rice atakuwa afisa wa ngazi ya juu kabisa wa serikali ya Marekani kuizuru Tripoli katika kipindi cha zaidi ya miaka 50.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Sean McComark amesema ukifiria juu ya muda huo wamekuwa na mtu alietuwa mwezini,mtandao,kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na wamekuwa na marais 10 wa Marekani kwa hiyo ziara hiyo ni muhimu hasa na ya kihistoria.

Anasema inaonyesha kwamba nchi zina chaguo na kwamba Libya imechaguwa kuwa na uhusiano tafauti na Marekani wenye tija kadhalika na jumuiya ya kimataifa.

Maandalizi ya ziara hiyo ya Rice yalikamilishwa mwezi uliopita wakati Libya ilipokubali kutowa mamilioni ya dola kwa kuzifidia familia za wale waliofariki katika uripuaji wa ndege ya shirika la ndege la Pan Am mwaka 1988 juu ya anga la Lokerbie nchini Scotland.

Majasusi wa Libya walihusishwa katika mripuko huo uliouwa watu 270 wakiwemo Wamarekani 189. Marekani na Libya zilisaini makubaliano hapo Augusti 14 na Marekani inataraji fedha hizo zitahamishiwa kwenye mfuko huo hivi karibuni.

Makubaliano hayo yanakomesha hatua zozote zile za kisheria dhidi ya serikali ya Libya katika mahkama za Marekani na yanajumuisha familia za wahanga wa Marekani wa mripuko wa mwaka 1986 wa klabu ya disko mjini Berlin ambao umeuwa wanajeshi wawili wa Marekani, mwanamke mmoja wa Kituruki na kujeruhi zaidi ya watu 200.

Rais wa wakati huo Ronald Reagan aliamuru mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya miji miwili ya Libya ya Tripoli na Benghazi ambayo yameuwa madarzeni ya watu akiwemo mtoto wa kike wa kulea wa Gaddafi wakati wa kushambuliwa kwa makao ya rais huyo.

Uamuzi wa Marekani wa kurudisha uhusiano na Libya na ziara hiyo ya Rice hapo kesho baada ya kusimama kwa muda nchini Ureno umezikasirisha familia za wahanga wa ndege ya Pan Am ambao bado wanamuona Gaddafi kuwa ni muuaji ambaye hapaswi kufaidika na uhusiano mzuri na Marekani.

Utawala wa Bush pia umeshutumiwa na makundi ya haki za binaadamu ambayo yanaamini kwamba Marekani imekuwa ikifumbia macho ukiukaji wa haki za binaadamu wa serikali ya Libya kwa matlaba ya biashara na kutaka kuungwa mkono katika vita dhidi ya ugaidi.

McComark amesema Rice anakusudia kuzusha mashaka ya haki za binaadamu wakati wa kukutana na Gaddafi.

Baada ya kuitembelea Libya Rice ataelekea Tunisia,Algeria na Morocco.

 • Tarehe 05.09.2008
 • Mwandishi Mohmed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FBXn
 • Tarehe 05.09.2008
 • Mwandishi Mohmed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FBXn
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com