1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Westerwelle ziarani mjini Abu Dhabi

20 Aprili 2011

Mkutano wa kila mwaka wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya na wenzao wa baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba wazungumzia wimbi la mageuzi

https://p.dw.com/p/10x4M
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle mjini Abu DhabiPicha: picture alliance / dpa

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Gudio Westerwelle anashiriki hii leo katika mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa ulaya na baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba ,mjini Abu dhabi.Kabla ya hapo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani alikuwa ziarani mjini Cairo ambako alizungumzia juu ya "walakini" katika juhudi za kuleta demokrasia nchini Misri na kuhimiza maendeleo katika kuheshimiwa sheria na kuimarisha demokrasia.

Kimsingi huu ni mkutano unaoitishwa kila mwaka kati ya baraza la ushirikiano la mataifa ya Ghuba na mawaziri wa Umoja wa Ulaya.Safari hii lakini mkutano huo wa leo ni wa aina yake kwasababu umegubikwa na migogoro mitatu inayotokota katika nchi za kiarabu nchini Libya,Bahrain na Yemen.

Kuhusiana na kilio cha wapenda mageuzi katika za kiarabu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema:

"Democrasia na taifa linaloheshimu sheria ni kitu kimoja sawa na unavyo shikamana uchaguzi huru na uhuru wa mtu kutoa maoni yake."

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa serikali kuu ya Ujerumani amehimiza papatikane ufumbuzi wa kisiasa haraka nchini Libya.

Libyen Rebellen Feuer
Mapigano nchini LibyaPicha: picture alliance/dpa

Mwanasiasa huyo wa kutoka chama cha kiliberali cha FDP amesema mjini Abu Dhabi ni muhimu watu wakiondokana na fikra ya kutanguliza mbele ufumbuzi kwa njia ya kijeshi.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa serikali kuu ya Ujerumani amehimiza ufumbuzi upatikane kwa kushirikishwa nchi jirani.Ametetea pia umuhimu wa kuendelezwa vikwazo."Libya inaweza kujipatia mustakbal mwema,huru na wa amani bila ya Gaddafi amesema waziri wa mambo ya nchi za anje wa serikali kuu ya Ujerumani na kuongeza upande huo,Umoja wa Ulaya na baraza la ushirikiano la mataifa ya Ghuba wana msimamo wa aina moja.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amezungumza pia na muakilishi mkuu wa siasa ya nje wa umoja wa ulaya bibi Catherine Ashton pamoja pia na mwenyeji wa mazungumzo haya ya Abu Dhabi,waziri wa mambo ya nchi za nje wa falme za nchi za kiarabu-Sheikh Abdullah bin Zayyed al Nahayan.

Westerwelle trifft Sharaf
Waziri wa nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na waziri mkuu wa Misri Essam SharafPicha: picture-alliance/dpa

Baraza la nchi za Ghuba linazileta pamoja Bahrain,Qatar,Kuweit,Oman,Saud Arabia na Falme za nchi za kiarabu.

Kabla ya Abu Dhabi,waziri wa mambo ya nchi za nje wa serikali kuu ya Ujerumani alikuwa ziarani mjini Cairo ambako aliahidi Ujerumani itaendelea kuiunga mkono serikali ya mpito ya Misri katika juhudi zake za kuleta demokrasia nchini humo.

Mwandishi:Kühntopp Carsten/Dubai(WDR)/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed