1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa elimu na sayansi apokonywa shahada ya uzamili

6 Februari 2013

Chuo kikuu cha Heinrich-Heine cha Dusseldorf kimempokonya waziri wa elimu na sayansi Anette Schavan wa chama cha CDU,shahada yake ya uzamili aliyoipata miaka 33 kwa makosa ya udangayifu

https://p.dw.com/p/17YmC
Mkuu wa kitivo cha falsafa katika chuo kikuu cha Dusseldorf Bruno BleckmannPicha: dapd

Baada ya miezi kadhaa ya uchunguzi kupitia vituo tofauti, wanachama15 wa baraza la kitivo cha falsafa walikutana kwa saa kadhaa jana na kukubaliana kwa wingi mkubwa bibi Anette Schavan,mwenye umri wa miaka 57 amefanya udanganyifu alipoandika tasnifu yake,aliyoipa jina "Mtu na Moyo."Schavan amefanya makusudi kutumia vifungu vya maneno na fikra ambazo kusema kweli si zake" amesema mkuu wa kitivo cha falsafa cha chuo kikuu cha Heinrich Heine mjini Düsseldorf,Bruno Bleckmann.

Waziri huyo wa elimu na sayansi wa serikali kuu ya Ujerumani daima amekuwa akisema pengine amefanya makosa ya kijuu juu,lakini hajafanya uhadaa wala udanganyifu.

Bibi Anette Schavan ambae hivi sasa yuko ziarani nchini Afrika kusini anajikuta hivi sasa mikono mitupu-shahada zake zote alizopata chuo kikuu zimekuwa batil baada ya kupokonywa shahada hiyo ya uzamili.

 Sauti zinapazwa

Annette Schavan Dissertation Doktorarbeit Plagiat
Waziri wa elimu na sayansi Annette SchavanPicha: picture-alliance/dpa

Wakili wake anasema watauandama uamuzi huo mahakamani.Washirika  katika chama cha Christian Democratic wameelezea kumuunga mkono waziri huyo katika hatua zote atakazochukua.Naibu kiongozi wa kundi la wabunge wa vyama vya CDU/CSU bungeni Michael Kretschmer anazungumzia juu ya kampeni ya kisiasa dhidi ya waziri huyo anaesifiwa zaidi miongoni mwa mawaziri wa serikali kuu ya Ujerumani.

Mtaalam wa masuala ya elimu  kutoka chama cha FDP  Patrick Meinhardt anasisitiza hadi uamuzi wa mahakama utakapopitishwa waziri Schavan anahaki ya kuangaliwa kuwa "hana hatia."

Upande wa upinzani lakini unamtaka waziri Anette Schavan ajiuzulu.Hata hivyo mwenyekiti wa achama cha Social Democratic Suigmar Gabriel anasema."Chuo kikuu kilichofanya uchunguzi kina sababu zake ambazo hazistahiki kuwekewa suala la kuuliza.Hata hivyo anasikitika sana.Anasema  anamthamini sana bibi Schavan,lakini madhara ya aina gani yanatokana na uamuzi uliopitishwa,anadhani yeye mwenyewe ndiye anaestahiki kutafakari."

Schavan asema hatojiuzulu

Annette Schavan und Angela Merkel Archivbild
Waziri Annette Schavan na kansela Angela Merkel (kulia)Picha: Reuters

Kwa mujibu wa ripoti za hivi punde bibi Schavan anasema hatojiuzulu.Pindi angeamua kujizulu hilo lingekuwa pigo kubwa kwa kansela Angela Merkel,miezi tisa kabla ya uchaguzi mkuu.Bibi Schavan anaangaliwa kama mshirika mkubwa wa kansela Merkel na mhimili muhimu wa serikali yake.Miaka miwili iliyopita kansela Merkel alimpoteza waziri mwengine kwasababu ya udanganyifu katika shahada ya uzamili.Wakati ule alikuwa waziri wa ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg wa kutoka chama cha CSU.

Mwandishi:Werkhäuser,Nina/Hamidou Oummilkhheir

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman