1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Steinmeier akamalisha ziara yake Marekani

Charo Josephat4 Februari 2009

Mwanzo wa enzi mpya wa uhusiano kati ya Marekani na Ulaya

https://p.dw.com/p/Gmu1

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amekamilisha ziara yake ya Marekani ambako alikutana mwenzake wa Marekani Hillary Clinton mjini Washington. Viongozi hao walijadiliana kuhusu Iran, Afghanistan na Mashariki ya Kati.

Siku moja tu baada ya waziri wa kigeni wa Marekani Hillary Clinton kuanza rasmi kazi yake, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier alikuwa na haraka ya kukutana naye. Hata hivyo hakuwa wa kwanza kuzungumza na Bi Clinton kwani waziri wa kigeni wa Uingereza alifaulu kuwa mbele na kukutana na Clinton kabla ya Steinmeier. Jambo hili hata hivyo halikumsumbua waziri Steinmeier ambaye kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na Bi Clinton katika wizara ya mambo ya ndani mjini Washington jana jioni, alionekana ameridhika.

Waziri Steinmeier amesema ziara yake ya Marekani ilikuwa ya kirafiki na inadhihirisha kwamba Ujerumani ni mojawapo wa washirika wa karibu wa Marekani. Amesisitiza kwamba katika mwaka mmoja uliopita, hajawahi kuwa na mazungumzo na serikali ya Marekani ambapo maswala mengi yanaoana na yale ya serikali ya Ujerumani.

Mazungumzo kati ya Steinmeier na Clinton yaliyodumu muda wa saa mbili na nusu, hayakutuwama tu juu ya urafiki bali pia mlolongo wa mizozo ya kimataifa na uhusino kati ya Marekani na Ulaya. Waziri Steinmeier amesema Ujerumani itaendelea kuiunga mkono Marekani katika maswala mengi, lakini alidokeza kabla ya ziara yake huenda kuwe na msimamo tofauti kuhusu mambo fulani, kama vile swala la Afghanistan.

Rais wa Marekani Barack Obama amelipa kipaumbele swala la kuimarisha usalama nchini Afhanistan na Marekani inataka kuongeza idadi ya wanajeshi nchini humo. Kuna uwezekano wa Ujerumani kuombwa itume wanajeshi wake zaidi kwenda Afghanistan, lakini hata hivyo waziri wa kigeni wa Marekani Hillary Clinton hajataka kuthibitisha hilo.

''Serikali yetu inachunguza upya sera yetu kuelekea Afghanistan. Mjumbe wetu maalum, balozi Richard Holbrook, atalitembelea eneo hilo juma lijalo na baadaye tutashauriana na marafiki zetu kuhusu tunachoweza kufanya pamoja.''

Pia kuhusu swala la jela ya Guantanamo waziri Hillary Clinton alioneka kusita. Waziri Frank Walter Steinmeir tayari amezunguzia uwezekano wa Ujerumani kuombwa kuwachukua baadhi ya wafungwa wa jela hiyo ya kijeshi ya Marekani nchini Cuba. Bi Clinton hata hivyo ameeleza kwamba serikali ya Marekani haijakuwa tayari kufanunua hatua zinazonuiwa kuchukuliwa.

''Naelewa wasiwasi iliyonao Ujerumani na mataifa mengine, lakini huu sio wakati mwafaka wa sisi kuiwasilishia Ujerumani au nchi nyingine maombi maalum. Wakati haujafika bado.''

Marekani ikishirikiana na Ujerumani zinataka kushauriana kuhusu njia za kuifanya Iran kutimiza majukumu yake ya kimataifa. Waziri Clinton amedokeza kuwa rais Barack Obama anataka kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Iran, lakini amesisitiza kutakuwa na athari iwapo Iran haitaheshimu maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, IAEA.

Waziri Frank Walter Steinmeier ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Iran kutengeneza satelaiti yake ya kwanza.

''Ikiwa kuna ujuzi wa kiufundi wa hali ya juu namna hii, basi tunalazimika kuwa macho zaidi na katika majuma na miezi ijayo tuongeze juhudi za kuishughulikia Iran.''

Waziri Steinmeier na waziri Clinton pia wamezungumzia njia ya kuwa na sera ya pamoja na Urusi kutanzua mizozo ya Afghanistan, Iran na Georgia.

Hii leo wajumbe wa Marekani, Urusi, China, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani wanakutana mjini Wiesbaden hapa Ujerumani kujadili njia za kukabiliana na mzozo wa nyuklia wa Iran.