1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Waziri mwingine Uganda apelekwa rumande kwa wizi wa mabati

17 Aprili 2023

Mahakama ya rushwa nchini Uganda imemsukuma rumande waziri wa nchi wa fedha na mipango baada ya kusomewa mashtaka ya kupatikana na mabati yaliokusudiwa kama msaada kwa jamii za wafugaji wa kuhamahama eneo la Karamoja.

https://p.dw.com/p/4QCYj
Uganda Kampala | Präsident Yoweri Museveni
Picha: SNA/IMAGO

Waziri huyo ambaye alitumia mabati hayo kuezeka vibanda vyake vya mbuzi na kuku alikamatwa mwishoni mwa wiki huku mawaziri wenzake wawili wakijificha ndani ya majengo ya bunge kukwepa kukamatwa na polisi.

Picha za vibanda vya mbuzi na kuku vilivyoezekwa kwa mabati yaliyodaiwa kuwa sehemu ya shehena ya mabati ya Karamoja zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii miezi miwili iliyopita.

Soma pia: Mahakama ya Uganda yamfungulia mashtaka ya ufisadi Waziri Kitutu

Mabati hayo yalidaiwa kua mali ya seikali iliyoibwa na waziri wa nchi wa fedha na mipango ya kiuchumi Amos Lugoloobi. Hii iliibua mjadala mkubwa kuhusu kashfa hiyo, wengi wanamitandao wakimshtumu waziri huyo kwa kutumia mabati yaliyokusudiwa jamii ya wafugaji wa kuhamahama.

Siku ya Jumatatu waziri huyo alifikishwa kizimbani na kusomewa mashtaka na jaji. Waziri Lugolobi amekanusha mashtaka mawili aliyosomewa ya kupokea na kupatikana na mali ya wizi.

Klimakrieg in Karamoja Hunger Dürre
Eneo la Karamoja ni mmoja ya yanayokabiliwa na umaskini mkubwa nchini Uganda.Picha: Simone Schlindwein

Museveni aahidi kuwawajibisha waliohusika na wizi

Waziri huyo alikamatwa mwishoni mwa wiki na kuzuiliwa hadi leo alipofikishwa mahakamani. Mawaziri wengine wawili wanawake waliopangiwa kukamatwa walijificha ndani ya majengo ya bunge kukwepa operesheni hiyo. Kulingana na ofisi ya kiongozi wa mashtaka, hadi sasa wameandaa mashtaka dhidi ya mawaziri 8.

Waziri wa kwanza kukamatwa wiki mbili zilizopita alikuwa Goretti Kitutu anayeshughulikia masuala ya Karamoja na siku ya Jumatano aliachiwa kwa dhamana.

Akigusia kashfa hiyo ya wizi wa mabati inahusisha mawaziri wake 22 na wabunge 31, wiki iliyopita Rais Yoweri Museveni alitaja vitendo vyao kama ufisadi wa kisiasa. Alisema kuwa atawachukulia wote waliohusika hatua za kisiasa ambazo zimefasiliwa na watu mbalimbali kuwa  yamkini atawafuta kazi.

Utapiamlo miongoni mwa watoto kanda ya Karamoja Uganda

Ila hayo yataweza kuwa maamuzi mazito kwani waliohusika ni mawaziri wanaoshikilia nyadhifa nyeti ikiwemo waziri mkuu na waziri wa fedha.

Ombi la mawakili wa waziri huyo kuachiwa kwa dhamana kutokana na hali yake ya afya na umri mkubwa lilipingwa na kiongozi wa mashtaka akisema kuwa mashtaka hayo ni ya ufisadi na pana haja ya kupata muda wa kutosha kukamilisha uchunguzi.

Ameongezea kuwa wanahitaji pia muda wa kutosha kuwahakiki wadhamini. Jaji amamsukuma gerezani rumande hadi tarehe 20 mwezi huu ambapo mahakama itatoa maamuzi kama aachiwe kwa dhamana.