Waziri mkuu wa Yemen anayeishi uhamishoni atembelea Aden | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri mkuu wa Yemen anayeishi uhamishoni atembelea Aden

Waziri mkuu wa Yemen anayeishi uhamishoni Khaled Bahar ametembelea mji ulioharibiwa kwa vita wa Aden, miezi kadhaa baada ya mashambulizi ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia kuanza dhidi ya waasi wa Kihuthi.

Jemen Regierungschef Bahah besucht Aden

Waziri mkuu wa Yemen Khaled Bahah akiwa mjini Aden

Waziri mkuu wa Yemen Bahah aliwasili mjini Aden akiwa na mawaziri sita wa serikali jana Jumamosi (01.08.2015) na kuondoka siku hiyo hiyo, kwa mujibu wa mkuu wa uwanja wa ndege wa mjini Aden Tarek Abdu Ali.

Msemaji wa serikali ya Yemen iliyoko uhamishoni , Rageh Badie, amesema ziara ya Bahah ina lengo la kuweka hali ya kawaida kwa maisha ya watu mjini Aden. Amesema Bahah amefahamishwa juu ya hali ilivyo na utendaji wa serikali za mitaa, na kuongeza kwamba serikali inafanyakazi kurejesha huduma.

Jemen Regierungschef Bahah besucht Aden

Waziri mkuu Khaled Bahah

Badie amesema Bahah , ambaye pia ni makamu wa pili wa rais nchini Yemen , amefanya ziara ya mji huo na kuangalia uharibifu uliosababishwa na miezi ya mapigano.

Waziri mkuu atathmini uharibifu

Wakati huo huo , jeshi na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wamepata udhibiti wa mji muhimu upande wa kusini wa Zanjibar, maafisa wa usalama wamesema pamoja na watu walioshuhudia.

Ali Hawasah, kamanda anayeunga mkono serikali akizungumza kwa simu kutoka Zanjibar, amesema wapiganaji wake wameingia katika mji huo na wanawasaka wapiganaji wa Kihuthi. Ameongeza kuwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wanasonga mbele wakipata msaada wa mashambulizi ya anga ya ndege za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia huku kukiwa na mapigano makali na wapiganaji waasi.

Jemen Luftangriff auf Mocha

Uharibifu katika mji wa Aden baada ya mashambulizi ya anga

Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wanalenga kupata udhibiti wa mji wa Zanjibar ili kuuweka mji wa Aden salama kutoka upande wa magharibi na kuzuwia njia muhimu ya kupata mahitaji kwa Wahuthi.

Maafisa wa Kihuthi wamesema wapiganaji wao wanaendelea kudhibiti eneo la magharibi na kusini la mji huo.

Mapigano yasambaa katika miji ya Yemen

Mapigano pia yameendelea katika mji wa tatu nchini Yemen wa Taiz, yakiuwa kiasi ya wapiganaji 65 kila upande katika muda wa siku mbili, maafisa wa hospitali na usalama wamesema.

Raia tisa pia wameuwawa mjini Taiz kutokana na mapigano hayo, maafisa hao wamesema.

Jemen Taiz Humanitäre Hilfe

Misaada ya kiutu ikitolewa katika mji wa Taiz

Maafisa hao wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kwasababu hawana ruhusa ya kuzungumza na waandishi habari.

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukifanya kampeni ya mashambulizi ya anga tangu Machi dhidi ya Wahuthi , ambao wanadhibiti mji mkuu Sanaa, sehemu za Yemen kaskazini na ambao wanajaribu kupanua eneo lao upande wa kusini wa taifa hilo masikini la Kiarabu lililoko katika rasi ya Arabuni.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape

Mhariri: Sudi Mnette

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com