Waziri Mkuu wa Uturuki na familia yake kwenda Somalia | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.08.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri Mkuu wa Uturuki na familia yake kwenda Somalia

Jumuiya ya Mataifa ya Kiislam leo inaanza mkutano wake wa dharura huko Istanbul Uturuki kujadiliana jinsi ya kusaidia kukabiliana na hali mbaya ya ukame na njaa katika pembe ya Afrika.

default

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan

Nchi wanachama 57 za jumuiya hiyo zinakutana kufuatia ombi la Uturuki ambayo ndiyo mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa sasa, ili kujadiliana jinsi ya kuimarisha misaada kwa wahanga wa baa la njaa katika eneo hilo.

Mkutano huo unafanyika huku Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akitarajiwa kuondoka kesho kwenda Mogadishu Somalia akiandamana na Waziri wa Mambo ya Nje Ahmed Davutoglu pamoja na familia zao.

Viongozi hao watakwenda kuangalia jinsi usambazaji wa misaada ya Uturuki nchini Somalia unavyokwenda.Tayari Uturuki imekwishatuma ndege tatu zenye shehena ya misaada ya chakula na madawa kwa wasomali wakati wa mwezi huu mtukukufu wa Ramadhani.

Viongozi wa serikali za dunia kutembelea Mogadishu ni nadra sana kutokana na usalama hafifu.Lakini Waziri huyo mkuu wa Uturuki ambaye amekuwa shujaa miongoni mwa viongozi wa kiislamu kwa msimamo wake dhidi ya Israel, amesema ni vigumu kwao kubaki wakitazama tu jinsi maisha ya binaadamu yanavyohatarishwa barani Afrika.

Kiongozi wa mwisho kuutembele mji huo mkuu wa Somalia Mogadishu, ni Rais Yoweri Musevi wa Uganda Novemba mwaka jana.

Naye Abdifatah Abdi Noor ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia amesema ziara hiyo ya Bwana Erdogan nchini Somalia ni nafasi muhimu sana kwani itazidi kuitanabaisha dunia juu ya hali nchini Somalia.

Televisheni za Uturuki zimekuwa zikionesha picha za wahanga na hali mbaya ya njaa katika pembe ya Afrika, ikiwa ni katika harakati za kuhamasisha misaada kwa wahanga hao.

Katika kampeni za kukusanya fedha, zaidi ya Euro millioni 80 zimekwishakusanywa, kupitia kampeni mbalimbali zikiwemo matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya mbio za Marathon zikiongozwa na wanasiasa mashuhuri halikadhalika wacheza sinema maarufu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kiasi cha watu millioni 12 wako katika hatari ya kufa kwa njaa kwenye eneo la Pembe ya Afrika, huku Somalia ikiwa imeathirika zaidi.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/APF/Reuters

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com