Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson asubiriwa Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.08.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson asubiriwa Berlin

Waziri mkuu mpya wa Uingereza Boris Johnson anaanza ziara ndefu na tete mijini Berlin na Paris kwa lengo la kujaribu kuitetea fikra yake kuhusu Brexit au utaratibu wa kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu mpya wa Uingereza Boris Johnson anaanza ziara ndefu na tete mjini Berlin na baadae Paris na Biarritz nchini Ufaransa kwa lengo la kujaribu kuitetea fikra yake kuhusu Brexit au utaratibu wa kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Katika ziara yake hii ya kwanza ughaibuni , kama waziri mkuu wa Uingereza, mrithi huyo wa Theresa May anatarajiwa kuwasili Berlin saa kumi na moja za jioni ambako atapokelewa kwa hishma za kijeshi kabla ya kukutana  kwa mazungumzo na kansela Angela Merkel.

Viongozi hao wawili "wameshawahi kuzungumza kwa simu. Lakini kuketi pamoja katika meza ya mazungumzo na kuzungumzia Brexit na masuala mengine ya Umoja wa ulaya, ni jambo muhimu bila ya shaka" amesema hayo msemaji wa kansela Merkel akiashiria "hakuna makubwa yanayotegemewa".

Kesho waziri mkuu huyo wa Uingereza atakaribishwa Elysée na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambae anatetea msimamo shupavu zaidi kuliko kansela Merkel katika suala la Brexit.

Ziara hiyo ndefu itamalizikia Biarritz ambako Boris Johnson atahudhuria kwa mara ya kwanza mkutano wa viongozi wa mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda G7 utakaohudhuriwa pia na mfuasi mkakamavu wa Brexit, rais wa Marekani Donald Trump.

Umoja wa ulaya unapinga fikra ya kujadili upya suala la Brexit

Mwenyekiti wa baraza la ulaya Donald Tusk

Mwenyekiti wa baraza la ulaya Donald Tusk

Mazungumzo kati ya waziri mkuu wa Uingereza na kansela wa Ujerumani Angela Merkel na baadae na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron yanaonyesha yatakuwa magumu hasa kwasababu ya pengo linalowatenganisha viongozi hawa wawili wa Ulaya na waziri mkuu anaetaka kwa kila hali kuitoa nchini yake katika Umoja wa ulaya, ikilazimika bila ya makubaliano.

Kitovui cha majadiliano ni pendekezo la Boris Johnson la kujitoa katika Umoja wa ulaya hadi ifikapo October 31 inayokuja.

Katika barua aliyomtumia mwenyekiti wa baraza la ulaya Donald Tusk jumatatu iliyopita, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alitilia mkazo msimamo wake dhidi ya kifungu cha usalama kuhusu  mpaka wa Ireland , au "Backstop. Kifungu hicho kinazungumzia umuhimu wa kutorejeshwa tena mpaka kati ya Ireland mbili -jamhuri ya Ireland ambayo ni mwanachama wa Umoja wa ulaya na Ireland ya kaskazini ambayo ni jimbo la Uingereza. Katika barua hiyo Johnson anakitaja kifungu hicho kuwa si cha kidemokrasi na anakituhumu kuizuwia nchi yake kufanya biashara bila ya kujifungamanisha na kanuni za Umoja wa ulaya. Umoja wa ulaya umesema mara kadhaa makubaliano ya Brexit hayatojadiliwa upya.Na kansela Merkel pia amesema jana alipokuwa ziarani Island, anataraji "mapendekezo ya maana yatatolewa kuhusu kifungu cha Backsstop."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com