1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Lebanon Hariri akubali mwaliko wa Ufaransa

Isaac Gamba
16 Novemba 2017

Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri pamoja na familia yake wamealikwa nchini Ufaransa. Hayo ni kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Ufaransa  ambayo imethibitisha kuwa mwanasiasa huyo amekubali mwaliko huo. 

https://p.dw.com/p/2njWN
Saudi Arabien Ex-Premier Hariri kündigt Rückkehr in den Libanon an
Picha: Reuters/M. Azakir

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bonn ambako  alikuwa akihudhuria mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi, rais wa Ufaransa Emanuel Macron  alisema Hariri pamoja na familia yake wamealikwa kwa ajili ya kukaa nchini Ufaransa kwa siku chache tu lakini akasema alikuwa hampatii kiongozi huyo hifadhi ya kisiasa.

Macron amesema kuna haja ya kuwa na viongozi  ambao wako huru katika kutoa maoni yao  na kuongeza kuwa ni muhimu kwa Hariri kuweza kuendeleza mchakato wa kisiasa nchini mwake katika siku na wiki zijazo.

Tangazo hilo linakuja mnamo wakati waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean- Yves Le Drian  akiwa nchini Saudi Arabia  ambako anakutanha na Hariri pamoja na mfalme wa Saudia.

Hariri akitolea mfano wa Iran na kundi la Hezbollah kuingilia masuala ya ukanda huo alitangaza kujiuzulu wadhifa wake akiwa nchini Saudi Arabia na tangu wakati huo hajarejea nchini Lebanon na Rais wa Lebanon bado hajakubali kujiuzulu kwake.

Frankreich Strassburg - Emanuel Macron hält Rede vor dem Europarat
Rais wa Ufaransa Emanuel MacronPicha: picture-alliance/abaca/E. Cegarra

Rais wa Ufaransa Emanuel Macron hapo jana Jumatano alimualika Hariri na familia yake nchini Ufaransa huku kukiwa na madai kuwa Saudi Arabia inamshikilia kiongozi huyo kama mfungwa.

Kwa upande mwingine ofisi ya rais wa Ufaransa imesema  baada ya kuzungumza na mwana wa mfalme Mohammed bin Salman na waziri mkuu wa Lebanon  Saad al Hariri rais Macron ameamua kumualika mwanasiasa huyo pamoja na familia yake.

Hariri pasipo kutarajiwa alitangaza kujiuzulu wadhifa wake kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa kupitia Televisheni  nchini Saudi Arabia Novemba 4 na siku 11 zilizofuatia kumekuwepo na uvumi kuhusiana na hali ya waziri mkuu huyo wa Lebanon.

Hapo jana Jumatano rais wa Lebanon  Michel Aoun alisema Hariri alikuwa akizuiliwa na maafisa wa Saudi Arabia na kutaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa  kuingilia kati.  Aoun alikataa kukubali kujiuzulu kwa Hariri na kumtaka arejee Beirut.

 Hayo yanajiri huku Saudi Arabia ikikanusha kuwa Hariri alikuwa akishikiliwa.

 Rais wa Ufaransa Emanuel Macron tayari alikwishafanya ziara ya kushitukiza  nchini Saudi Arabia  Alhamisi iliyopita na kukutana na mwana wa mfalme Mohammed bin Salman mnamo wakati mivutano ikiibuka kati ya Saudi Arabia na Iran.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/ape

Mhariri  : Mohammed Abdul-Rahman