Waziri mkuu wa Israel ziarani mjini Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.01.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri mkuu wa Israel ziarani mjini Berlin

Kikao cha kwanza cha pamoja kati ya serikali ya Ujerumani na ile ya Israel mjini Berlin

default

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu (wa pili kutoka kushoto)na kansela Angela Merkel (wa pili kutoka kulia)

Kwa mara ya kwanza tangu vita vikuu vya pili vya dunia kumalizika, miaka 65 iliyopita, serikali ya Ujerumani na serikali ya Israel zimekutana kwa kikao cha pamoja katika ofisi ya kansela mjini Berlin. Lengo ni kutoa ishara ziada ya suluhu kati ya nchi hizi mbili. Mada kuu mazungumzoni ni pamoja na juhudi zinazozorota za amani ya mashariki ya kati na mzozo uliosababishwa na mradi wa kinyuklea wa Iran.

Waziri mkuu Benjamini Netanyahu amewasili mjini Berlin akifuatana na ujumbe mkubwa ikiwa ni pamoja na waziri wa ulinzi, Ehud Barack, waziri, mambo ya nchi za nje, Avigor Liebermann, na msaidizi wake, Danny Ayalon.

Kwa pamoja, kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na ujumbe wake wametembelea kumbusho la wahanga wa mauwaji ya halaiki mjini Berlin. Eneo lote la kumbusho hilo, karibu na lango la Brandenburger, lilizingirwa na vikosi vya polisi ili kuepukana na wafanya fujo.

Mada kuu wakati wa mazungumzo hayo ni pamoja na mpango wa kinyuklea wa Iran .Israel inataka kuhakikisha juhudi za Iran za kujipatia silaha za kinuklea hazizai matunda.

Kansela Angela Merkel ameshawahi kufanya ziara kama hii pamoja na mawaziri wake mjini Jerusalem miaka miwili iliyopita, na kuhusu suala hilo kansela Angela Merkel alisema wakati ule :

"Ujerumani sawa na washirika wake inapendelea ufumbuzi kwa njia ya kidiplomasia. Ikiwa Iran haitoregeza kamba, Ujerumani itapigania kuwekwa vikwazo zaidi dhidi ya Iran."

Mada nyengine zilizojadiliwa ni pamoja na miradi ya pamoja kuhusu utafiti na namna ya kuendeleza nishati mbadala, misaada kwa nchi zinazoinukia na zaidi kuliko yote ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizi mbili.

Duru kadhaa za mazungumzo kwa daraja ya mawaziri zimefanyika pia pembezoni mwa mazungumzo hayo. Mawaziri wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle, na Avigdor Liebermann wamekubaliana kuzidisha uhusiano wao katika sekta ya utamaduni. Duru za karibu na mazungumzo hayo zinasema mawaziri hao wawili wamezungumzia pia mzozo wa mashariki ya kati-lakini hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa.

Shirikisho la jamhuri ya Ujerumani ni mshirika wa pili muhimu wa Israel baada ya Marekani. Serikali ya Israel sawa na vyombo vya habari nchini humo vinathamini sana uungaji mkono wa Ujerumani katika sekta ya kisiasa na tekenolojia ya kijeshi kwa Israel. Benjamini Netanyahu,sawa na mtangulizi wake, wanategemea mengi kutoka serikali kuu ya Ujerumani.

Ziara hii iliyokua awali ifanyike November 30 mwaka jana, iliakhirishwa kutokana na sababu za afya ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Mwandishi. Clemens Verenkotte/Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na: Miraji Othman

:

 • Tarehe 18.01.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LYv3
 • Tarehe 18.01.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LYv3
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com