1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Irak akutana na kansela wa Ujerumani

Charo, Josephat22 Julai 2008

iongozi hao wamezungumzia njia za kuimarisha uchumi kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/Ehxj
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na waziri mkuu wa Irak Nouri al-Maliki mjini BerlinPicha: AP

Kansela wa Ujeruamni Angela Merkel amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki mjini Berlin hii leo. Katika ziara ya kwanza hapa nchini Ujerumani ya kiongozi huyo wa Irak, serikali ya Ujerumani imeweka wazi kwamba inataka kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na serikali ya mjini Baghdad.

Ujerumani ina ubalozi wake mjini Baghdad, ambao umetatizwa katika utendaji wake kutokana na kuwa nje ya eneo lililo salama linalolindwa na Marekani la Green Zone. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani imetangaza itafungua ubalozi mdogo nchini Irak mwaka ujao utakaosimamiwa na mwanadiplomasia wa ngazi ya juu mjini Arbil katika eneo la wakurdi la kaskzini mwa Irak.

Baada ya mazungumzo yake na kansela Merkel, waziri mkuu wa Irak Nuri al Maliki amesema Irak inaweza kusimamia usalama wake na iko tayari kwa uwekezaji mkubwa wa kigeni. Kiongozi huyo amesisitiza Irak imepiga hatua kubwa katika maswala ya usalama akiongeza kuwa wakati huu kuna uhuru na demokrasia nchini Irak.

Nuri al Maliki amesema mojawapo ya malengo la ziara yake ya siku mbili hapa Ujerumani ni kuibadili taswira ya Irak. Wakati wa ziara yake hiyo kiongozi huyo wa Irak atakutana pia na viongozi wa biashara.

Nuri al Maliki amewataka wakimbizi wote Wairaki wanaoishi Ujerumani warejee Irak akisitiza kwamba Wairaki wakristo wana mahala pa kuishi nchini humo. Kumekuwa na wasiwasi hapa Ujerumani kuhusu jinsi wakristo nchini Irak wanavyoshughulikiwa na kumetolewa miito na baadhi ya wanasiasa kuwa maombi ya wakristo wa Irak kutaka vibali vya kuishi Ujerumani yapewe kipaumbele.

Kansela Merkel ameyatumia mazungumzo yake na waziri mkuu Nuri al Maliki kupata anayoyatarajia kiongozi huyo kutoka nchi za Ulaya na pia kuyafufua mahusiano ya jadi kati ya serikali ya mjini Berlin na serikali ya Baghdad. Bi Merkel amesema Ujerumani iko katika nafasi ya kubadilishana ujuzi wake wa kiteknolojia na raslimali za Irak. Ujerumani inaweza kutumia ujuzi wake kuunda serikali ya shirikisho ambao Irak ilikuwa ikiunda kwa kuwapa mafunzo wafanyakazi wa serikali.

Kansela Merkel amesema Irak ina historia ya kiviwanda ambayo inaweza kutumiwa wakati kampuni za Ujerumani zitakapoingia soko la Irak. Axel Nitschke, kiongozi wa biashara ya nchi za kigeni wa muungano wa viwanda na biashara wa hapa Ujerumani, DIHK, amesema biashara za Ujerumani zina nafasi kubwa ya kufanya vizuri nchini Irak.

Ujerumani ilipinga vikali vita dhidi ya Irak vilivyoongozwa na Marekani mnamo mwaka wa 2003 kumuondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein. Lakini tangu wakati huo imekuwa ikiisaidia Irak kujenga upya vikosi vyake vya usalama na kuendeleza uchumi.

Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael Glos alifanya ziara ya kushangaza mjini Baghdad mwezi huu na hivyo kuwa waziri wa kwanza wa Ujeruamni kuzuru mjini humo tangu Irak ilipovamiwa mnamo mwaka wa 2003.