1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Waziri mkuu wa Haiti atakiwa kuhojiwa kwa mauaji ya rais

Mohammed Khelef
11 Septemba 2021

Mwendesha mashitaka mkuu nchini Haiti amemtaka Waziri Mkuu Ariel Henry kuelezea sababu za kuzungumza kwa simu na mmoja kati ya washukiwa wa mauaji ya Rais Jovenel Moise usiku wa tukio lenyewe tarehe 7 Julai 2021. 

https://p.dw.com/p/40BXU
Haiti I  Ariel Henry wird Premierminister
Picha: Matias Delacroix/AP/picture alliance

Barua ya mwaliko iliyoandikwa kwa maneno ya hadhari inasema Henry alizungumza mara kadhaa kwa simu na mshukiwa mkuu wa mauaji ya Rais Mose, Joseph Felix Badio, wakati mshukiwa huyo, ambaye bado anatafutwa, alipokuwa bado karibu na eneo la mauaji.

Barua hiyo iliyotumwa na mwendesha mashitaka, Bed-Ford Claude, kwa waziri mkuu huyo siku ya Ijumaa (Septemba 10) inasema "ingawa ni rais pekee ndiye mwenye mamlaka ya kuamuru kuitwa kwenye mahojiano kwa mtu mwenye cheo chako, lakini kwa sasa Haiti haina raisi, nami nakualika kuhudhuria na kutowa ushirikiano."

Claude alimwambia waziri mkuu kwamba angependa kuonana naye kuthibitisha mazungumzo yake na Badio, ingawa aliashiria kwamba halikuwa jambo la lazima kwake kukubali mwaliko huo.

Mahojiano hayo yatafanyika Jumanne ijayo (14 Septemba) saa 4:00 asubuhi kwenye Mahakama ya Kwanza ya mji mkuu, Port-au-Prince. 

Rais Moise alipigwa risasi na kuuawa wakati wauaji walipoingia nyumbani kwake Julai 7 mwaka huu, tukio lililoliingiza taifa hilo fukara la Carrebean kwenye mkwamo zaidi wa kisiasa. 

Uhusiano wa Henry na Badio

Haiti I Beerdigung von Präsident Jovenel Moise
Mazishi ya Jovenel Moise yaliyofanyika tarehe 23 Julai 2021.Picha: Orlando Barria/Agencia EFE/imago images

Chenal Augustin, afisa wa mawasiliano kwenye ofisi ya waziri mkuu, alikataa kusema chochote juu ya mwaliko huo wa mwendesha mkuu wa mashitaka. 

Licha ya wachunguzi kusema wanaamini Badio ndiye aliyeamuru kufanyika mauaji hayo, hivi karibuni Henry alikiambia kituo kimoja cha televisheni kwamba anamjuwa Badio na alimtetea kwamba asingeliweza kuhusika "kwa kuwa hakuwa na njia za kufanya hivyo."

Maarten Boute, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya Digicel Haiti, aliliambia shirika la habari la AP kwamba kampuni yake ililazimika kukabidhi taarifa za mawasiliano hayo kama zilivyoombwa na mahakama, lakini alikataa kusema mengi zaidi, akisisitiza kwamba ni jambo la siri.

Mwaliko wa kumuhoji Henry umetolewa katika wakati ambapo mamlaka zinawasaka washukiwa wengine wa mauaji hayo, akiwemo Badio, aliyewahi kufanyia kazi wizara ya sheria na kisha kujiunga na kitengo cha kupambana na ufisadi mwaka 2013.

Zaidi ya washukiwa 40 wameshatiwa nguvuni, wakiwemo wanajeshi 18 wa zamani kutoka Columbia, ambao hivi karibuni wamewatuhumu polisi wa Haiti kwa kuwatesa. 

Mwezi uliopita, jaji aliyekuwa ameteuliwa kusimamia kesi hiyo alijiuzulu akitaja sababu binafsi, ingawa uamuzi wake ulifanyika siku chache baada ya mmoja wa wasaidizi wake kufa katika mazingira ya kutatanisha.