Waziri Mkuu wa China ziarani Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri Mkuu wa China ziarani Ulaya

Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao leo ameanza ziara yake ya siku saba barani Ulaya itakayompeleka katika nchi tano.Hiyo kesho atahudhuria Jopo la Kimataifa la Uchumi mjini Davos Uswissi.

Chinese Premier, Wen Jiabao, applauds as he addresses the opening session of the National People's Congress held at the Great Hall of the People in Beijing, Wednesday, March 5, 2008. China's premier called Wednesday for powerful measures to rein in inflation that is battering ordinary Chinese and warned of risks from a global slowdown and the U.S. credit crisis. (AP Photo/Ng Han Guan)

Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao.

Hivi sasa ulimwengu mzima ukikabiliwa na mzozo wa fedha,ni dhahiri kuwa masuala ya uchumi yatachukua nafasi ya juu kabisa hata atakapokwenda Berlin, Brussels, Madrid na London.Lakini uhusiano kati ya China na Ulaya una matatizo yake.

Kwa kweli ziara ya Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao barani Ulaya ilipangwa kufanywa miezi miwili iliyopita kuhudhuria mkutano wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na China mjini Lyon.Lakini ghafula China iliivunja ziara hiyo,kwa sababu Peking ilihamakishwa na Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy ambae wakati huo alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Ulaya.Kwani Sarkozy licha ya upinzani mkali wa China,aliamua kukutana na kiongozi wa kidini wa Tibet Dalai Lama nchini Poland .Na tarehe 4 Desemba Dalai Lama alipokewa kwa shangwe katika Bunge la Ulaya. Wakati huo rais wa bunge hilo Hans Gert-Pöttering alisema:

"Bunge la Ulaya linatambua mipaka ya China,Tibet ikiwemo ndani ya mipaka hiyo.Lakini daima tutatetea haki ya watu wa Tibet kuwa na uhuru wa kufuata utamaduni na dini yao.Daima tutatetea haki hiyo."

Lakini baada ya majuma machache tofauti hizo za maoni hazikusikika sana. Badala yake habari zilizochomoza zilihusika na mzozo wa uchumi na fedha ulioenea kote duniani.Na sasa ziara ya waziri mkuu wa China inaelezwa kuwa ni ziara ya imani.Hata Umoja wa Ulaya imeacha kupaza sauti. Kibiashara Umoja wa Ulaya ni mshirika mkubwa kabisa wa China. Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita biashara kati ya pande hizo mbili imeongezeka zaidi ya maradufu na kufikia kama Euro bilioni 300. Lakini biashara hiyo inaelemea zaidi upande mmoja.Kwa mfano katika mwaka 2007 biashara ya Ulaya nchini China ilikuwa na nakisi ya Euro bilioni 160 na pengo hilo linazidi kuwa kubwa.Kwa maoni ya Eberhard Sandschneider,mtaalamu wa masuala ya China katika shirika la Kijerumani kuhusu siasa za nje,tatizo kuu katika uhusiano wa Ulaya na China ni uhaba wa uratibu ndani ya Umoja wa Ulaya.Na hiyo hutumiwa na China kwani imetambua kuwa Umoja wa Ulaya kibiashara ni mshirika muhimu lakini kisiasa umoja huo hauna msimamo mmoja.Na hilo ni tatizo la Ulaya na sio China.

 • Tarehe 27.01.2009
 • Mwandishi M.von Hein - (P.Martin)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GhQL
 • Tarehe 27.01.2009
 • Mwandishi M.von Hein - (P.Martin)
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GhQL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com