1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria pia ang'atuka.

Mtullya, Abdu Said1 Oktoba 2008

Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Günther Beckstein pia ameamua kujiondoa kufuatia matokeo mabaya ya uchaguzi ya chama chake.

https://p.dw.com/p/FSOy
Waziri Mkuu wa Bavaria Günther Beckstein aliejiuzulu.Picha: AP


Siku nne  baada ya chama chake CSU kushindwa  vibaya katika uchaguzi ,waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Günther Beckstein leo ametangaza kujiuzulu.

Bwana  Beckstein ameeleza kwamba baada ya chama chake kupoteza  kura nyingi  katika uchaguzi  wa jimbo , sasa haoni  kuwa anaungwa mkono na chama  hicho, kwa kiasi  cha kumwezesha  kuunda  serikali ya mseto.

Waziri mkuu  Beckstein alifahamisha juu ya uamuzi  wake wa kujiuzulu kwenye kikao maalumu  cha  chama  chake mapema leo katika  mji mkuu wa Bavaria, Munic baada ya wawakilishi wa mikoa kadhaa  wa  chama hicho kumtaka bwana Beckstein  ang'atuke.


Bwana Beckstein ameeleza kuwa amejiuzulu kwa sababu  chama  chake hakimwuungi mkono baada ya kushindwa vibaya  sana katika uchaguzi wa  jumapili iliyopita.

Waziri mkuu huyo wa  jimbo la Bavaria lililopo kusini  mashariki  mwa Ujerumani ameeleza  kuwa itakuwa vigumu kutekeleza majukumu yake katika serikali ya mseto ya jimbo lake ikiwa haungwi mkono na chama  chake kwa kiasi  cha kutosha.  


Kwa mujibu  wa duru za ndani ya chama cha CSU,mwenyekiti mteule wa chama hicho bwana Horst Seehofer huenda akachukua wadhifa wa waziri mkuu vilevile ,wa jimbo hilo la Bavaria lenye nguvu kubwa  za kiuchumi kuliko Sweden.

Lakini habari zaidi kutoka mji mkuu wa Bavaria Munic zinasema wanasiasa kadhaa wa chama cha  CSU wanapinga wazo la bwana Seehofer ambae pia ni waziri wa kilimo na maslahi ya wateja katika serikali  kuu, ya Ujerumani  kuwa waziri mkuu  wa  Bavaria. Badala yake wanasiasa hao ikiwa pamoja na  Spika wa bunge la Bavaria  wanataka  mtu mwengine  awe waziri mkuu.  Hatahivyo bwana Seehofer na waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann kadhalika, wamesema kuwa wapo tayari ,kuziba pengo lililoachwa na bwana  Günther  Beckstein.Wanasiasa wengine wawili  wa chama cha  CSU pia wanawania nafasi hiyo.

Waziri mkuu wa  jimbo  la  Rheinland -Palatinate  bwana Kurt Beck amesema ni wazi kwamba bwana   Beckstein amejizulu kutokana  matokeo mabaya sana  ya uchaguzi wa jumapili iliyopita katika jimbo la Bavaria.

Katika uchaguzi huo chama cha CSU kilipoteza  viti     zaidi ya 30  na hivyo kupoteza nafasi ya kuwa mtawala wa pekee katika jimbo la Bavaria kwa mara ya kwanza  baada ya  miaka 40. Kujiuzulu  kwa  bwana  Beckstein kunafuatia kujiuzulu  kwa  mwenyekiti wa  chama hicho  cha CSU  hapo  jana Erwin huber.