Waziri Kabudi asema Gwanda alitoweka na kufariki | Matukio ya Afrika | DW | 11.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Waziri Kabudi asema Gwanda alitoweka na kufariki

Suala la kutoweka kwa mwandishi wa habari Azory Gwanda nchini Tanzania limechukua mwelekeo mwingine baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo, Profesa Palamagamba Kabudi kusema kuwa mwandishi huyo “alitoweka na kufariki”.

Sikiliza sauti 02:32

Waziri Kabudi amesema hayo wakati alipohojiwa na kituo cha utangazaji cha BBC akiwa mjini London hapo jana.  Akijibu suali lililotaka kufahamu hatma ya mwandishi huyo aliyetoweka tangu septamba 2017,Waziri Kabudi ambaye ni msomi wa sheria alinukuliwa akisema kwamba visa vya watu kutoweka vimesababisha uchungu mwingi nchini humu.

''Wacha nikwambie unapozungumzia kuhusu kisa hicho, ni mojawapo ya visa ambavyo vimesababisha uchungu mwingi nchini Tanzania," alisema waziri huyo.

Waziri Kabudi pia amesema kwamba katika eneo la Rufiji sio tu Azory Gwanda aliyetoweka na kufariki, na anataka kukuhakikishia kwamba serikali inachukua kila hatua sio tu katika eneo la Rufiji bali pia maeneo mengine ya Tanzania ili kuhakikisha watu wako salama na sio tu waandishi bali pia Polisi na raia wa kawaida.

Muda mfupi baada ya mahojiano hayo kuruka hewani, makundi ya wanaharakati wa haki za binadamu walianza kusambaza mitandaoni sehemu ya mahojiano wakimtaka Waziri huyo kueleza familia ya mwandishi huyo sehemu uliko mwili wake na kubainisha jinsi alivyofariki dunia.

Wakati wanaharakati hao wakiendelea kuzua mjadala kwenye mitandao, nayo Kamati ya ulinzi wa wanahabari CPJ, imetoa wito kwa serikali ya Tanzania kutoa maelezo ya kina kuhusu hatima ya mwandishi huyo wa kujitegemea. Kwa mujibu wa kamati ya CPJ, hadi sasa serikali haijatoa maelezo kufuatia ahadi yake ya kuchunguza kisa hicho. 

Ama wakati matamshi hayo ya waziri Kabudi yakiendelea kujadiliwa, kumekuwa na ripoti kwamba waziri huyo ambaye pia alifanya mahojiano kwa lugha ya Kiswahili amenukuliwa akisema kile alichokitamka katika lugha ya kiingereza siyo msimamo wake rasmi.

Baadhi ya watetezi wa haki za binadamu hata hivyo wanaendelea kusisitiza kuhusu kauli yake ya awali na wakimtaka ajitokeza hadharani kubainisha bayana kile anachokijua kuhusu mwandishi huyo.

Hata hivyo, mmoja ya wanaharakati kutoka mtandao wa kutetea haki za binadamu Onesmo Olengurumwa aliyezungumza na DW amesema kuwa Waziri Kubudi amesisitiza kuhusu kubadili kauli yake. Azory Gwanda alitoweka Novemba 21, 2017 baada ya kufuatilia habari kuhusu mauaji ya kutatanisha pamoja na kutoweka kwa watu miongoni mwa jamii yake.