1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawili wauwa, 20 wajeruhiwa Lubumbashi kuelekea uchaguzi DRC

Mohammed Khelef
12 Desemba 2018

Zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, taarifa zinasema wafuasi wawili wa mgombea wa upinzani wameuawa katika makabiliano na polisi jimboni Katanga.

https://p.dw.com/p/39vOE
Präsidentschaftskandidat der Demokratischen Republik Kongo, Martin Fayulu
Picha: Getty Images/A. Huguet

Kwa mujibu wa shirika la haki za binaadamu la ACAJ la nchini Kongo, watu 43 walijeruhiwa, 15 kati yao kwa risasi, kwenye mkutano wa jana kwenye mji mkuu wa jimbo la Katanga, Lubumbashi, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini humo. Askari polisi mmoja pia anaripotiwa kujeruhiwa vibaya.

Polisi inasema maafisa wake 11 na raia wawili walijeruhiwa kwenye makabiliano na wafuasi wa Martin Fayulu, mgombea wa muungano wa upinzani, Lamuka, ambao umesema watu waliouawa ni sita.

Mwandishi wa habari ya shirika la AFP aliyekuwepo kwenye eneo la tukio anasema polisi walirusha mabomu ya machozi kuwatawanya mamia ya watu waliokuwa wamekusanyika kumpokea Fayulu, lakini mfanyabiashara huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 62 na mbunge asiyefahamika sana, anasema kuwa polisi walitumia silaha za moto kumzuwia kutumia uwanja aliopanga kukutana na wafuasi wake kwa ajili ya kampeni.

"Polisi walitulazimisha kufuata mipangilio yao na kutuzuwia kufika uwanjani. Walitupeleka kwenye nyumba ya Papa Kyungu," alisema Fayulu akikusudia kiongozi wa upinzani wa Lubumbashi.

Shirika la haki za binaadamu la Kongo, ACAJ, lilisema wafuasi 27 wa Fayulu walikamatwa na polisi, ambao kabla ya hapo walikuwa wamewachawanya watu waliojitokeza uwanja wa ndege wa Lubumbashi kumpokea Fayulu.

Wasiwasi wazidi

Kollage von den vier Top-Kandidaten DR Kongo
Baadhi ya wanasiasa wanaowania urais kwenye uchaguzi wa Disemba 23 nchini Kongo.

Kumekuwa na wasiwasi wa ghasia kuelekea uchaguzi wa tarehe 23, ambapo wapigakura watachaguwa mrithi wa rais wa sasa, Joseph Kabila, mwenye miaka 47 na aliyeendelea kubakia madarakani kama rais wa mpito licha ya muhula wake wa pili na wa mwisho kumalizika miaka miwili iliyopita. 

Kongo, taifa lenye utajiri mkubwa wa madini na ambalo halijawahipo kushuhudia makabidhiano ya madaraka kwa njia za amani tangu kupata uhuru wake kutoka mkoloni wa Kibelgiji mwaka 1960, lina wagombea 21 wa urais kumrithi Kabila, ambaye amekuwa madarakani tangu Januari 2001, baada ya kuuawa baba yake, Laurent-Desire Kabila.

Mwezi uliopita, Fayulu aliteuliwa kuwania kwa niaba ya vyama kadhaa vya upinzani, akikabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa mgombea mwengine wa upinzani, Felix Tshisekedi, na yule wa vyama tawala anayeungwa mkono na Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary.

Mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa Fayulu ni Moise Katumbi, gavana wa zamani wa Lubumbashi na mwenye ngome yake huko, ingawa mwenyewe amezuiwa kushiriki uchaguzi huu. Lakini Lubumbashi ipo kwenye jimbo la kusini magharibi la Katanga, ambalo pia ni ngome ya Kabila na ndiko mgombea wake, Shadary, alikozinduwa kampeni zake tarehe 23 mwezi uliopita wa Novemba.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga