1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu watatu wauawa Syria

Aboubakary Jumaa Liongo19 Agosti 2011

Vikosi vya jeshi la Syria vimewaua waandamanajai 3, mnamo wakati ambapo maelfu ya waandamanaji wakiingia mitaani mara baada ya swala ya Ijumaa na kuzidisha upinzani wao dhidi ya serikali ya Rais Assad kumtaka ajiuzulu

https://p.dw.com/p/12KKc
Vikosi vya Syria vikipiga doria katika mji wa SaqbaPicha: AP

Kwa upande mwengine, mbinyo unazidi kutoka kwa viongozi mbalimbali duniani kumtaka Rais Assad ang´atuke.

Kwa mujibu wa shirika moja la haki za binaadamu nchini Syria, liitwalo Observatory for Human Rights, watu watatu waliuawa na wengine 16 kujeruhiwa katika jimbo la Daraa lililoko kusini mwa Syria.Lakini shirika la habari la Syria, SANA, limesema kuwa polisi pamoja raia wameuawa na watu waliyokuwa na silaha huko Daraa.

Takriban watu elfu 20 pia inaripotiwa kuwa wameingia mitaani kuandamana huko katika mji wa Al-Khalidiyen uliyo jirani na mji wa Homs, ambao ndiyo kitovu cha upinzani huo dhidi ya serikali. Maandamano ya leo yamepewa jina: Ijumaa ya mwanzo wa ushindi.

Mjini Washington, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amesema nchi hiyo inamtaka Rais Assad aondoke haraka madarakani.

Hata hivyo, Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Bashar Jaffar, ameishutumu Marekani na mataifa mengine ya magharibi kwa kuwatumia magaidi kutaka kuiangusha serikali ya nchi hiyo.

Urusi na Uturuki ni nchi ambazo zimekataa kuunga mkono wito wa kumtaka Rais Assad aondoke madarakani.

Shirika la habari la Urusi, Interfax, limemnukuu afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo, akisema kuwa haiungi mkono wito huo,na kuongeza kuwa serikali ya Assad inatakiwa kupewa muda wa kutekeleza mchakato wa mabadiliko iliyotangaza kutaka kuyafanya.

Mjini Ankara, serikali ya Uturuki imesema wito wa kumtaka Rais Assad aondoke madarakani ni lazima utoke kwa wananchi wenyewe wa Syria, na kuongeza kuwa mpaka sasa upinzani haujaonesha kuuangana na kutoa wito wa pamoja kutaka kuondoka kwa kiongozi huyo.

Hata hivyo, mapema leo wapinzani hao ambao wamekiri kutokuwa na umoja wametangaza kuanzishwa kwa kile walichokiita kamisheni kuu ya mapinduzi nchini Syria.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/ZPR

Mhariri:Othman Miraji