Watu wanane wauawa Atlanta, wengi wao wana asili ya Asia | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

ATLANTA

Watu wanane wauawa Atlanta, wengi wao wana asili ya Asia

Watu wanane, miongoni mwao wanawake sita wenye asili ya Asia, wameuawa katika jimbo la Georgia nchini Marekani, huku mashambulizi dhidi ya watu wa jamii hiyo yakiongezeka kufuatia dhana potofu juu ya virusi vya corona.

Wanne miongoni mwao waliuawa kwenye saluni ya uchuwaji viungo kwenye kiunga cha Atlanta, karibu na mji mkuu wa jimbo hilo la Georgia.

Mkuu wa Kaunti ya Cherokee, Kapteni Jay Baker, aLIsema wahanga hao walikuwa ni wanawake wawili wenye asili ya Asia, mwanamke mmoja Mzungu, na mwanamme mmoja Mzungu, huku mwanamme mwengine mwenye asili ya Kihispania akijeruhiwa.

Polisi pia iLIthibitisha kuuawa kwa wanawake wengine wanne kwenye matukio mengine mawili tafauti, kaskazini mashariki mwa mji huo, ambapo walisema walipofika eneo la tukio waliwakuta wanawake watatu wakiwa wameshapoteza maisha kutokana na majeraha ya risasi.

Vile vile, polisi walisema wakati wakiwa kwenye eneo hilo, walisikia milio ya risasi mtaani na kufika wakamkuta mwanamke mwengine akiwa ameshauawa.

Wote wanne walikuwa Wamarekani wenye asili ya Asia.

Mshukiwa atiwa nguvuni

USA | Schießerei in Massagesalons in Atlanta

Eneo la tukio ambako watu wanne waliuawa mjini Atlanta, Georgia.

Polisi ilitaja jina la mshukiwa wa mauaji yote hayo kuwa ni Robert Aaron, kufuatia uchunguzi wa kamera za siri kwenye maeneo yaliyofanyika mashambulizi.

"Kwa sasa tunashughulikia kesi za marehemu wanne na majeruhi mmoja. Mshukiwa ametambuliwa kuwa ni Robert Aaron Long mwenye umri wa miaka 21, anayeishi kwenye Kaunti hii ya Cherokee. Tumechapisha picha yake na kwa sasa yupo kizuizini." Alisema mkuu wa Kaunti ya Cherokee, Jay Baker.

"Walimkamata kwa mbinu na bila matatizo," alisema Baker, akiongeza kwamba walikuwa wanachunguza iwapo mshukiwa huyo alikuwa na mawasiliano na watu wengine katika kufanya mashambulizi hayo.

Wamarekani wenye asili ya Asia walengwa

USA | Schießerei in Massagesalons in Atlanta

Eneo la tukio ambako watu wanne waliuawa mjini Georgia, Atlanta.

Shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap, limeripoti kwamba wizara ya mambo ya kigeni ya nchi hiyo imethibitisha kuwa wanne kati ya waliouawa walikuwa na asili ya Korea.

Mauaji haya yamefanywa wakati ripoti za mashambulizi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Asia, hasa watu wazima, zikiongezeka kutokana na dhana potofu juu ya maradhi ya COVID-19, ambayo wanaharakati wanasema imechochewa na kauli ya rais wa zamani, Donald Trump, kuviita virusi vya corona kuwa ni "Virusi vya Kichina".

Uchunguzi wa maoni uliofanywa baina ya Machi 2020 na Februari mwaka huu unaonesha takribani asilimia 70 ya Wamarekani wenye asili ya Asia wamewahi kukabiliwa na kauli za matusi na mmoja katika kila kumi amewahi kushambuliwa kimwili. 

Jimbo la Georgia lina wakaazi wapatao 500,000 wenye asili ya Asia, ambao ni sawa na asilimia nne ya wakaazi wote wa jimbo hilo.