Watu waachwa bila makaazi kufuatia tetemeko la ardhi Rubavu | Masuala ya Jamii | DW | 26.05.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Watu waachwa bila makaazi kufuatia tetemeko la ardhi Rubavu

Mitetemeko ya ardhi inaendelea kushuhudiwa nchini Rwanda hasa katika mji wa Rubavu unaopakana na DRC na kuwalazimisha wengi kuyakimbia makazi yao hasa baada ya kutokea mpasuko wa ardhi uliougawa mji huo siku ya Jumatatu

Ni siku ya tatu tangu ardhi ya mji wa Rubavu kukumbwa na mpasuko. Bizimana Sylvestre ni mmoja wa waathirika mkazi wa kata ya Byahi ambapo ndipo mpasuko umeanzia. Nyumba yake kwa sasa haikaliki.

Majira ya saa tatu usiku wa kuamkia leo amezungumza na DW akiwa amekaa nje na familia yake kwa kukosa malazi.

"Kiwanja changu kimegawanyika sehemu mbili, yaani nyumba ambayo nilikuwa naishi mimi na familia yangu huku ikiwa pia na vyumba vitano vya wapangaji sote tuko nje nimewakataza watoto kurudi ndani isiwaangukie. Chakusikitisha zaidi wapangaji wanasema lazima niwarudishie kodi. Sebule iliyokuwa na marumaru imepasuka huku kuta pia zikionekana kuwa na nyufa," alisema Bizimana Sylvestre.

soma zaidi: Gesi ya sumu yauwa 7 Kongo baada ya volkano kuripuka

Serikali imeanza kuwahamisha wote ambao nyumba zao ziko katika umbali wa mita hadi mia mbili kutoka sehemu ya mpasuko wa ardhi, huku pia soko la mji wa Rubavu likifungwa.

Hali hiyo iliyoambatana na mfululizo wa mitetemeko ya ardhi imewafanya baadhi ya wakazi wa Rubavu kukimbilia wilaya jirani za Nyabihu na hata Musanze bila kusubiri kuhamishwa, ikiwa ni baada ya nyumba zao au zile za majirani zao na hata msikiti mmoja kuharibika.

Serikali inasema inatafuta suluhu ya changamoto raia wanazopitia

Karte DR Kongo EN

Ramani inayoonesha eneo la Congo na baadhi ya majirani zake

Gandika Nestor ni mwalimu wa Kiswahili katika shule moja iliyoko Rugerero mjini Rubavu, anasema watu wanakimbia kutoka mji huo kwenda wilaya nyingine, huku wengine wakionekana kulala nje. Gandika ameongeza kuwa wanaokimbia ni wanawake na watoto na wanaume wanabaki kuangalia hali itakavyokuwa lakini huenda watu wengi zaidi wakaondoka mjini humo.

soma zaidi: Goma yakabiliwa na uhaba wa chakula baada ya volkano

Waziri wa Mambo ya Ndani, Jean Marie Vianney Gatabazi, amewataka wananchi kutulia akisema serikali inayajua matatizo yao na inashughulika kuyapatia ufumbuzi.

"Hizo nyumba tumezitembelea na kiukweli zina nyufa kubwa, tumekubaliana na viongozi wa wilaya ya Rubavu kwamba familia kama 40 zitafutiwe mahali pengine pa kuishi kwa muda walau wa miezi mitatu wakati wenyewe wakitafuta uwezo wa kufanya ukarabati au namna nyingine ya kuendesha maisha yao,” alisema Waziri Jean Marie Vianney Gatabazi

Mitetemeko ya ardhi imepasua hata barabara zinazounganisha mitaa mbalimbali ya mji wa Rubavu na kuharibu baadhi ya shule kiasi kwamba wazazi wengine wamewazuia watoto wao wasiende shule ili zisiwawadondokee.

Janvier Popote, DW, Rubavu.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com