1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 6 wauawa Sudan licha ya muafaka kuhusu baraza la mpito

Daniel Gakuba
14 Mei 2019

Waandamanaji 5 na mwanajeshi mwenye cheo cha meja wameuawa nchini Sudan, katika mvutano ulioibuka jana, saa chache baada ya Baraza la kijeshi na viongozi wa waandamanaji kukubaliana juu ya taasisi za uongozi wa mpito.

https://p.dw.com/p/3ISGr
Sudan Proteste in Khartum
Picha: Reuters/M.N. Abdallah

Vifo hivyo vilitokea katika makabiliano mbele ya makao makuu ya jeshi la Sudan mjini Khartoum, ambako maelfu ya waandamanaji wameendelea kuweka kambi kwa wiki kadhaa, kulishinikiza jeshi kukabidhi madaraka kwa raia baada ya kuangushwa kwa Rais Omar al-Bashir.

Msemaji wa baraza la kijeshi lililojipa mamlaka ya kuongoza kipindi cha mpito, Luteni Jenerali Shams al-Deen Kabashi amesema katika mkutano na waandishi wa habari usiku wa kuamkia leo, kwamba watu wenye silaha wasiojulikana wamejipenyeza katika maandamano hayo, na ndio waliofyatua risasi.

Soma zaidi: Mahasimu Sudan Kusini wachelewa kuunda serikali

''Makundi kadhaa yakiwemo yanayounga mkono serikali iliyoangushwa wamejipenyeza kwa lengo la kuyahujumu mapinduzi,'' amesema Kabashi na kuongeza ''wameeneza uvumi, na siku mbili zilizopita walishambulia gari lililokuwa likigawa kifungua kinywa, na ni dhahiri jeshi halikuhusika.''

Malengo ya kuligawa jeshi

Sudan - Generalleutnant Shamseddine KabbashiSudan - Generalleutnant Shamseddine Kabbashi
Msemaji wa jeshi la Sudan, Lt. Gen. Shams el-Deen KabbashiPicha: Getty Images/M. El-Shahed

Msemaji huyo ameyashutumu makundi hayo kueneza uvumi kwa madhumuni ya kugonganisha jeshi na kitengo chake cha kuingilia haraka katika mizozo.

Amesema jeshi linaunga mkono maandamano, na kamwe halitowafyatulia risasi kwa sababu yoyote ile, ingawa pia halitavumilia matendo ya vurugu.

Vuguvugu la waandamanaji lijulikanalo kama ''Muungano kwa Ajili ya Uhuru na Mabadiliko'' limekubaliana na maelezo hayo ya jeshi, kwamba waliosababisha vurugu ni wafuasi wa serikali ya zamani, walio na malengo ya kukwamisha majadiliano kati ya vuguvugu hilo na jopo la majenerali.

Muafaka kuhusu taasisi za mpito

Mauaji hayo ya jana yalitokea baada ya jeshi na viongozi wa waandamanaji kuafikiana juu ya taasisi zitakazoiongoza nchi katika kipindi cha mpito. Kulingana na msemaji wa vuguvugu la waandamanaji Taha Osman, taasisi hizo ni baraza kuu, baraza la mawaziri pamoja na bunge.

Sudans Präsident Omar al-Bashir
Rais wa Sudan aliyepinduliwa, Omar al-Bashir ameshtakiwa mahakamaniPicha: Getty Images/A. Shazily

Hata hivyo, pande hizo mbili bado hazijakubaliana juu ya muundo wa taasisi hizo wala muda wake wa kuhudumu kabla ya uchaguzi.

Wakati wanajeshi wakishinikiza baraza la mpito lihudumu kwa muda wa miaka miwili, vuguvugu la waandamanaji linataka muda zaidi wa miaka minne.

Soma zaidi: Al Bashir kuhojiwa kwa utakatishaji fedha na ugaidi

Wakati haya yakiarifiwa, mwendeshamashtaka mpya wa Sudan Al-Waleed Sayyed Ahmed amesema rais wa zamani Omar al-Bashir na wasaidizi wake wameshitakiwa kwa uhalifu wa kuchochea vurugu na kushiriki katika mauaji dhidi ya waandamanaji. Mashtaka hayo yanahusiana uchunguzi juu ya mauaji ya daktari mmoja katika wilaya ya Burri Mashariki mwa mji mkuu, Khartoum.

Takwimu za mwezi uliopita za kamati ya madaktari zinasema watu 90 waliuawa katika maandamano haya ya Sudan yaliyoanza Desemba iliyopita, lakini idadi rasmi inayotolewa na mamlaka ni watu 65.

 

afpe,rtre