1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 70 wamekwama katika mizozo

Caro Robi
23 Januari 2018

Shirika la kimataifa la kutoa misaada ya kiutu la CARE limesema watu wasiopungua milioni 70 wamekwama katika mizozo ya kibinadamu ambayo haiangaziwi na wafanyakazi wa kutoa misaada, wafadhili na vyombo vya habari.

https://p.dw.com/p/2rLdW
Flüchtlinge im Südsudan
Picha: AFP/Getty Images/C. Lomodong

Ripoti hiyo ya Shirika la  CARE iliyopewa jina kuteseka kimya kimya imeangazia mizozo kumi ya kibinadamu ambayo haikuripotiwa kama inavyosatahili mwaka jana huku Korea Kaskazini, Eritrea na Burundi zikiwa nchi zilizo katika mstari wa mbele kuwa na mizozo ambayo haiangaziwi ipasavyo.

Kaimu katibu mkuu wa shirika la CARE Laurie Lee amesema baadhi ya mizozo hiyo ambayo ilihitaji kushughulikiwa kwa dharura ni kama hata haikuonekana. Amewaambia wanahabari kuwa ripoti walizozipokea zinaonesha takriban watu milioni 10 katika nchi kumo zinazokumbwa na mizozo wanataabika kimya kimya.

Somalia Mogadischu | Bishara Suleiman, ICRC Health Field Officer
Mfanyakazi wa shirika la misaada la ICRC nchini Somalia Picha: DW/S. Petersmann

Lee ameongeza kusema mizozo na majanga katika nchi hizo ambayo yanachangia theluthi moja ya watu milioni 220 wanaohitaji misaada ya kibinadamu duniani ilipokea tu asilimia mbili ya ufadhili. Nchini Korea Kaskazini asilimia 70 ya raia hawapati chakula cha kutosha na wanategemea misaada ya chakula kutoka kwa Serikali.

Hiyo inamaanisha watu milioni 18 nchini humo wanakabiliwa na kitisho cha uhaba wa chakula lakini suala hilo halikuangaziwa vilivyo na mashirika ya kutoa misaada, wafadhili hawakulishughulikia na vyombo vya habari havikuripoti kwa kina kuhusu mzozo huo.

Ripoti hiyo ya shirika la CARE inasema ulimwengu uliangazia zaidi kuhusu mzozo wa kinyuklia wa Korea Kaskazini na mzozo wa kisiasa, lakini si mengi yanayojulikana kuhusu hali ya kibinadamu inayojiri nchini humo.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, Wakorea Kaskazini wawili kati ya watano wanakumbwa na tatizo la kutopata chakula cha kutosha mwilini huku ikiripotiwa zaidi ya watoto laki mbili nchini humo wanakumbwa na utapia mlo mbaya.

Flüchtlinge im Südsudan
Mtoto wa miaka miwili anayeugua utapiamlo katika jimbo la Jonglei Sudan Kusini Picha: AFP/Getty Images/C. Lomodong

Korea Kaskazini inakabiliwa na majanga ya mara kwa mara kama mafuriko, ongezeko la joto na vipindi virefu vya kiangazi. Julai iliyopita, nchi hiyo ilikumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 2001.

CARE hairuhusiwi kuingia Korea Kaskazini ambako shirika la mpango wa chakula duniani WFP na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC ni miongoni mwa mashirika machache yaliyoruhusiwa kutoa misaada nchini humo.

Kati ya nchi kumi zilizotajwa kutekelekezwa, saba ni za Afrika nazo ni Eritrea, Burundi, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchi zinazozunguka ziwa Chad. Nchi nyingine zilizotajwa katika ripoti hiyo yan CARE ni Vietnam na Peru.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman