1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadhaa wauwawa katika moto wa jengo la ghorofa London

Admin.WagnerD14 Juni 2017

Moto umewaka kwenye jengo la ghorofa nyingi Magharibi ya London alfajiri ya Jumatano(13.06.2017) na kuuwa idadi ya watu isiojulikana na kujeruhi wengine zaidi ya hamsini waliopelekwa hospitali katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/2egPW
Großbritannien Großbrand in Londoner Hochaus
Picha: picture-alliance/Zumapress

Moto umewaka kwenye jengo la ghorofa nyingi Magharibi ya mji mkuu wa Uingereza London alfajiri leo hii na kuuwa idadi ya watu isiojulikana na kujeruhi wengine zaidi ya hamsini waliopelekwa hospitali katika eneo hilo.Mohamed Dahman anasimulia zaidi juu ya janga hilo ambapo mashahidi wamelezea watu walikuwa wakiruka kutoka maghorofani kunusuru maisha yao.

Nassima Boutrig mkaazi wa magharibi ya Londonn mmojawapo wa wakazi walioshudia janga hilo amesema "Katu sikuwahi kuona moto kama huo kabla.Hiii ni mara yangu a kwanza. Lakini kwa kweli ilikuwa inatisha na kwa kweli nilikuwa nalia wakati nilipouona moto huo.Nilitaka kusaidia lakini ningeliweza kusaidia vipi?Nusu ya jengo lilikuwa linaunguwa ,watu walikuwa wanalia,watu walikuwa wakipiga kelele ngazini ghorofa ya 20 hali ikuwa mbaya.....mbaya kabisa!"

 

Inaelezwa kuwa moto huo ulikuwa ukitoka madirishani kwenye jengo la ghorofa 24 la Grefen Tower kaskazini mwa Kesington wakati zaidi ya wazima moto 200 walipokuwa wakipambana kuuzima.Ukungu wa moshi ulikuwa ukiweza kuonekana umbali wa maili kadhaa katika anga ya mji mkuu huo.

Kamishna wa kikosi cha kuzima moto Dany Cotton amewaambia waandishi wa habari hilo ni tukio ambalo halina kifani kwamba katika historia yake ya miaka ya 29 ya kuwa askari wa kuzima moto katu hakuwahi kushuhudia kitu kama hicho yaani moto wa kiwango kikubwa kiasi hicho.

Idadi ya waliokufa haijuikani

Großbritannien Großbrand in Londoner Hochaus
Hali ya jengo baada ya moto kudhibitiwa kwa kiasi fulani.Picha: picture-alliance/empics/V. Jones

Cotton amesema watu kadhaa wamekufa kutokana na moto huo lakini kamishna huyo ambaye ni mwanamke hakuweza kuthibitisha ni watu wangapi waliopoteza maisha yao kutokana na ukubwa wa moto wenyewe na kwa ugumu wa jinsi jengo lenyewe lilivyojengwa.

Mashahidi wamesema wameona watu wakiruka kutoka ghorofa za juu.David Blanco mkaazi wa jengo jirani na eneo la tuko amesema amemuona mtu mmoja akijaribu kuruka nje ,mmoja aliruka hasa nje na hicho ndicho kilichotokea na ilikuwa ni jinamizi

Chanzo cha moto hakijulikani

Großbritannien Großbrand in Londoner Hochaus
Wazima moto wakipumuwa.Picha: picture-alliance/AP/dpa/M. Dunham

Kikosi cha zima moto cha London kilipata taarifa za kwanza kuhusu moto huo saa saba kasoro dakika sita hivi usiku na magari ya kwanza ya kuzima moto yaliwasili katika kipindi kisichozidi dakika sita.

Sababu ya moto huo haikuweza kujulikana mara moja.Wakaazi wanasema inaonekana moto huo ulianzia katika nyumba ya ghorofa ya chini ya jengo hilo na kusambaa maghorofani kwa haraka.

Jengo hilo la Grenfell Tower lilijengwa mwaka 1974 na lina nyumba 120 lilikarabatiwa hivi karibuni kwa gharama ya pauni milioni 8 ambapo kazi ya kulikarabati ilimalizika mwezi wa Mei.

Shirika la Grenfel Action Group ambalo ni shirika la kijamiii llioundwa kupinga kuendelezwa kwa eneo karibu na hapo limekuwa likitahadharisha juu ya hatari ya jengo hilo tokea mwaka 2013.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP

Mhariri:Yusuf Saumu