Watu bilioni moja duniani wakabiliwa na njaa | Masuala ya Jamii | DW | 11.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Watu bilioni moja duniani wakabiliwa na njaa

Ufukara, migogoro na ukosefu wa amani ni mambo yaliyosababisha watu wapatao bilioni moja duniani katika mwaka huu wa 2010 peke yake wakumbwe na balaa la njaa, wengi wao wakiwa katika Afrika na Asia

Mtoto akiramba sufuria la chakula, dalili ya njaa na ukosefu wa lishe bora

Mtoto akiramba sufuria la chakula, dalili ya njaa na ukosefu wa lishe bora

Ripoti ya mashirika matatu ya kimataifa yanayojihusisha na masuala ya njaa duniani: Taasisi ya Kimatiafa ya Utafiti wa Sera ya Chakula, Concern Wordlwide na Welthungerhilfe, inasema kwamba, kati ya nchi 122 zilizotajwa kwenye Faharisi ya Njaa Ulimwenguni mwaka huu, nchi 25 ziko kwenye kiwango cha hali ya tahadhari na ambapo nne kati ya nchi za Afrika, zipo kwenye kiwango cha juu zaidi cha hatari.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nchi yake ina kiwango cha juu cha njaa

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nchi yake ina kiwango cha juu cha njaa

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, inashikilia nafasi ya juu kwenye faharisi hiyo. Robo tatu ya wakaazi wa nchi hiyo, wana kiwango cha chini kabisa cha lishe; na idadi ya vifo vya watoto ni kubwa kuliko nchi yoyote ulimwenguni. Ripoti hiyo inasema kwamba mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe ulioanza kuikumba DRC katika miaka ya '90, ulipelekea kuporomoka kwa uchumi, watu kuyahama makaazi yao wakikimbia vita na, kwa hivyo, kusababisha ukosefu wa usalama wa chakula.

Nchi nyengine zilizo kwenye hali mbaya sana ya njaa ni pamoja na Haiti, Burundi, Comoro, Eritrea na Chad, ambazo nazo ama ziliwahi au zimeendelea, kuwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe. Katika nchi hizi, zaidi ya asilimia 50 ya watu wake wana kiwango cha chini cha lishe.

Nchi za Bangladesh, India, Timor ya Mashariki na Yemen zinatajwa kwenye ripoti hiyo kwamba zina kiwango kikubwa cha watoto wenye uzito mdogo. Zaidi ya asilimia 40 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana tatizo hilo.

Nchi za Angola, Chad na Somalia zimewekwa kwenye orodha ya nchi zenye kiwango kikubwa cha vifo vya watoto, ambapo zaidi ya asilimia 20 ya watoto hufariki kabla ya kufikia umri wa miaka mitano.

Korea ya Kaskazini, Gambia, Swaziland na Zimbabwe ni miongoni mwa nchi tisa ambazo rekodi yao ya kiwango cha njaa ilipanda juu zaidi kutoka alama 16.2 mwaka 1990 hadi alama 19.4 mwaka huu. Nchi hizi zinahusishwa na ama migogoro ya ndani na au tawala za mkono wa chuma.

Nchi nyengine zilizo kwenye faharisi hii ya njaa ni pamoja na Nepal, Tanzania, Cambodia, Sudan, Burkina Faso, Togo, Guinea-Bissau, Rwanda, Djibouti, Msumbiji, Liberia, Zambia, Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Madagascar, Sierra Leone na Ethiopia.

Tanzania na Djibouti hazijawahi kukumbwa na migogoro mikubwa ya wenyewe kwa wenyewe, lakini ni miongoni mwa nchi masikini duniani, licha ya kuwepo kwa utajiri mkubwa wa rasilimali katika mataifa hayo.

Faharisi ya Njaa Ulimwenguni inatumia mambo matatu katika kupima kiwango cha njaa kwenye nchi husika, yaani ulinganifu wa watu wenye lishe ya hali ya chini, idadi ya watoto wenye uzito mdogo na kiwango cha vifo vya watoto.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 11.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pb2e
 • Tarehe 11.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pb2e
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com