1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 9 wauawa kwenye shambulizi Chad

Grace Kabogo
22 Septemba 2021

Watu tisa wameuawa katika shambulizi lililotokea kwenye kijiji kilicho karibu na Ziwa Chad, ambacho kinakumbwa na ghasia zinazofanywa na makundi ya jihadi.

https://p.dw.com/p/40eCI
Tschad | Armeesoldaten in N'Djamena
Picha: AFP/Getty Images

Gavana wa eneo hilo, Mahamat Fadoul Mackaye amesema wapiganaji wa Boko Haram wamekishambulia kijiji cha Kadjigoroum na kuwaua watu tisa na kukichoma moto kijiji hicho usiku wa Jumapili.

Mkuu wa shirika moja lisilo la kiserikali ambaye hakutaka kutajwa jina, amethibitisha kuhusu shambulizi hilo na idadi ya watu waliouawa.

Mwezi Agosti, wanajeshi 26 waliuawa katika shambulizi lililofanywa na Boko Haram kwenye kisiwa cha Tchoukou Telia cha Ziwa Chad, kilichoko umbali wa kilomita 190 kaskazini mwa mji mkuu wa Chad, N'Djamena.

Eneo hilo linapakana na Niger, Nigeria na Cameroon na wapiganaji wa Boko Haram na kundi hasimu la wapinzani linalojiita Dola la Kiislamu katika kanda ya Afrika Magharibi, ISWAP yamekuwa yakilitumia kulishambulia jeshi na raia.