1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 60 wafa Mexico kwa tetemeko la ardhi

Mohammed Khelef
9 Septemba 2017

Mexico imetangaza siku tatu za maombolezo, baada ya moja ya matetemeko makubwa kabisa kuwahi kutokea kulikumba eneo la kusini mwa nchi hiyo, likiyaangusha majengo na kuangamiza maisha ya watu zaidi ya 60.

https://p.dw.com/p/2jcpn
Mexiko Erdbeben
Picha: Reuters/E. Garrido

Tetemeko hilo lililopiga usiku wa kuamkia Ijumaa (8 Septemba) lilikuwa kubwa mno kiasi cha kwamba hata majengo imara katika mji mkuu, Mexico City, yalitikisa, yakiwa umbali wa kilomita 1,000 kutoka kilipo kitovu cha tetemeko lenyewe. 

Rodrigo Soberanes, anayeishi karibu na San Cristobal de las Casas jimbo la Chiapas lilikotokea tetemeko hilo anasema nyumba yake "iliyeyuka kama ubani wa kutafuna."

Tetemeko hili limeikumba Mexico wakati ikiwa inapambana na madhara ya Kimbunga Katrina upande mwengine wa nchi. Mvua kubwa zimeripotiwa kwenye jimbo la Veracruz, ambako upepo mkali wa Kigawe 2 ulitarajiwa kuzidi Ijumaa jioni au mapema Jumamosi. 

Rais Enrique Pena Nieto alisema kuwa watu 61 wamekufa kutokana na tetemeko hilo - 45 katika jimbo la Oaxaca, 12 Chiapas na 4 Tabasco. Mji ulioharibiwa zaidi ni Juchitan, ambako watu 36 walikufa. Nusu ya mji huo umegeuzwa kifusi na mitaa imejaa mabaki ya nyumba za raia.

Hospitali moja pia ilianguka, kwa mujibu wa Rais Pena Nieto aliyetembelea mji huo na kukutana na wakaazi wa huko. Wagonjwa wamehamishiwa maeneo mengine.

Rais huyo alisema kuwa mamlaka zinashughulikia kurejesha huduma ya maji na chakula na kutoa matibabu kwa wale wanaohitaji. Aliahidi kuwa serikali yake ingeliwasaidia waathirika kujijenga upya, huku akitoa wito wa umoja.

Hurricane Irma Luftaufnahme Kuba Florida
Kimbunga Irma chaelekea Cuba kutokea Marekani.Picha: picture-alliance/NOAA via AP

"Nguvu ya kimbunga hiki ilikuwa kubwa mno, lakini tuna hakika kwamba nguvu ya umoja, nguvu ya mshikamano na nguvu ya kushirikiana itakuwa kubwa zaidi," alisema Pena Nieto.

Ingawa mji mkuu, Mexico City, ulinusurika na madhara makubwa, wakaazi wake walilazimika kukimbia huko na huko mitaani usiku wa manane, wengi wakikumbuka janga kama hilo la mwaka 1985, ambalo liliangamiza maisha ya maelfu ya wakaazi na kuiharibu sehemu kubwa ya mji huo.

Haya yanatokea wakati kimbunga chengine kwa jina Katia kikielekea mashariki mwa Mexico hivi leo (Jumamosi 9 Septemba). Hata hivyo, watabiri wa hali ya hewa wanasema tufani hiyo kilishuka hadi Kigawe 1 kwa kipimo  cha Saffir-Simpson, wakati kilipofika jimbo la Veracuz.

Hata hivyo, Kimbunga Irma kilichoipiga Marekani siku ya Ijumaa, sasa kimeingia Cuba kikiwa na Kigawe 5, cha juu kabisa na baada ya kuuwa watu 21 kwenye eneo la Carrebean pamoja na kuharibu majumba na miundombinu kadhaa.

Mamilioni ya wakaazi wa Florida wamehamishwa, wakati kimbunga hicho kikubwa kabisa kikitembea kwa kasi ya kilomita 260 kwa saa. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Sudi Mnette