Watu 420,000 wapoteza makaazi kufuatia mafuriko Sudan Kusini | Matukio ya Afrika | DW | 15.11.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Watu 420,000 wapoteza makaazi kufuatia mafuriko Sudan Kusini

Shirika la kimataifa la misaada la Save the Children limesema zaidi ya watu 420,000 wamelazimika kuondoka kwenye makaazi yao kutokana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko Sudan Kusini. 

Shirika hilo limesema, kiasi asilimia 60 ya walioondoka, tayari walikuwa wanakabiliwa na utapiamlo mkali, kabla ya kuanza kwa mvua hizo zisizo za kawaida mwezi Julai. 

Kwa ujumla, inakadiriwa watu 900,000 ama asilimia 7 ya idadi jumla ya watu nchini humo wameathirika na mafuriko, hii ikiwa ni kulingana na shirika la Save the Children.

Aidha shirika hilo limeongeza kuwa ilikuwa ni vigumu kupeleka misaada ya uokozi kwa watu hao kutokana na mafuriko, hali iliyowalazimu kusitisha upelekaji  wa misaada kwenye baadhi ya maeneo. 

Mkurugenzi wa Save the Children nchini Sudan Kusini, Rama Hansraj, amesema mafuriko nchini humo yamefikia katika kiwango cha kutia wasiwasi na watoto pamoja na familia zao wanahitaji msaada wa dharura, katika wakati ambapo kunatarajiwa mvua nyingi zaidi wiki zijazo.