1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran Human Rights: Watu 31 wauawa kwenye maandamano Iran

23 Septemba 2022

Watu wasiopungua 31 wameuawa tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga kifo cha msichana mwenye umri wa miaka 22 aliyefariki akiwa mikonnoni mwa polisi wa kulinda maadili nchini Iran.

https://p.dw.com/p/4HEzu
Protest gegen den Tod von Mahasa Amini im Iran
Picha: AP/dpa

Taarifa hiyo imetolewa Jana na Shirika la kutetea haki za binaadamu la Iran Human Rights (IHR). Mkurugenzi wa Shirika hilo  Mahmood Amiry-Moghaddam amefahamisha katika taarifa baada ya siku 6 za maandamano kuwa wananchi wa Iran wameingia mitaani ili kutetea haki zao za msingi  lakini serikali inayazima maandamano hayo kwa kutumia risasi za moto.

Kituo cha habari cha serikali hata hivyo kimethibitisha vifo vya watu 17 huku mamlaka nchini Iran katika lengo la kuzuia kueneenea kwa maandamano hayo, imesitisha huduma ya mitandao ya kijamii kama Instagram na Whatsap ambayo hutumiwa na waandamanaji walio wengi na hii ikiwa ni hatua kali zaidi tangu mwaka 2019 kuliposhuhudiwa maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya petroli.

Soma zaidi: Raisi aonya waandamanaji nchini Iran

Katika nchi ambayo vituo vya redio na televisheni tayari vinadhibitiwa na serikali na ambako waandishi wa habari mara kwa mara wamekuwa wakikabiliwa na tishio la kukamatwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi limeitaka Mahakama leo kumshtaki ``mtu yeyote anayeeneza kwenye mitandao ya kijamii na kwengineko habari za uwongo na uvumi'' kuhusu maandamano hayo.

Hisia yaibuka kimataifa kufuatia kifo hicho

Kifo cha Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 kiliibua hisia na kukemewa kimataifa huku mashirika ya kimataifa yakikosoa matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji. Katika jukwaa la Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Marekani Joe Biden alidhihirisha mshikamano wake na wale aliyowaita ´´Wanawake majasiri wa Iran´´.

Soma zaidi: Kifo cha msichana Mahsa chazusha maandamano makubwa Iran

Iran | Protest gegen den Tod von Mahsa Amini in Teheran
Waandamanaji nchini Iran wakichoma pikipiki ya polisi kupinga mauaji ya mwanamke Mahsa Amin.Picha: WANA NEWS AGENCY/REUTERS

Mwanamke huyo mwenye asili ya Kurdistan alikamatwa na polisi ya kulinda maadili mjini Tehran Septemba 13 na kufariki akiwa hospitalini siku tatu baadaye baada ya kukutwa na kinachoitwa kosa la ´´kuwa na mavazi yasiyofaa´´, katika taifa ambalo wanawake wanalazimika kuficha nywele zao na hawana haki ya kuvaa nguo fupi, zinazobana au zilizochanika.

Sababu tofauti za kifo hicho zatajwa

Watetezi wa haki za binaadamu wenye mafungamano na Umoja wa Mataifa wanasema sababu za kifo cha mwanamke huyo ni majeraha aliyoyapata baada ya kupigwa kichwani, taarifa inayokanushwa na mamlaka za Iran zilizotaja kuwa sababu za kifo hicho ni mshtuko wa moyo na kwamba wameanzisha uchunguzi. 

Kifo cha Mahsa Amini kimezua shutuma kali kutoka Umoja wa Mataifa, Marekani na hata Umoja wa Ulaya.

Maandamano hayo yamezidi kuenea na kuwa changamoto kubwa kwa serikali, wakati wanawake wakiamua kuvua hijabu zao na kuzichoma moto huku wakitoa wito wa kuuangusha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

(AFPE, APE)