1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Watu 174 wamekufa katika mkanyagano nchini Indonesia

2 Oktoba 2022

Mkanyagano huo ulitokea katika mechi ya soka. Hadi sasa watu 174 ndio wameripotiwa kufariki na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa katika tukio hilo.

https://p.dw.com/p/4HebV
Indonesien | Unruhen am Kanjuruhan Stadion
Picha: Yudha Prabowo/AP/picture alliance

Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia 174 baada ya mkanyagano katika mechi ya soka nchini Indonesia. Vurugu zilizuka kati ya mashabiki wa timu mbili pinzani katika uwanja wa Kanjuruhan.

Idadi hiyo inaweza kuongezeka, kwani zaidi ya watu 300 wamejeruhiwa na wako katika hali mahututi.

Mamlaka za Polisi zisema rabsha zilijitokeza mara tu baada ya mchezo kumalizika kati ya Persebaya Surabaya iliyopata ushindi dhidi ya Arema Malang kwa mabao 3-2.

Indonesien | Unruhen am Kanjuruhan Stadion
Polisi wa Indonesia wakifyatua mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki wa soka huko Java, 01.10.2022Picha: Yudha Prabowo/AP/picture alliance

Polisi wa kutuliza ghasia walifyatua mabomu ya kutoa machozi, jambo ambalo lilizusha hofu miongoni mwa mashabiki waliojaribu kukimbia.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), tayari imeomba ripoti kamili juu ya tukio hilo baya lililotokea katika jiji la Java Mashariki. Chama cha soka cha Indonesia kimesimamisha ligi ili kufanya uchunguzi.

Kandanda ni mchezo unaopendwa zaidi nchini Indonesia lakini umekua ukigubikwa na vurugu za mashabiki ambapo kati ya mwaka 1994 hadi 2019, mashabiki 74 walikufa katika vurugu zinazohusiana na kandanda.