Watu 17 wauawa katika mapigano Somalia. | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Watu 17 wauawa katika mapigano Somalia.

Mapigano kati ya Wapiganaji na majeshi ya serikali magharibi mwa Somalia yamesababisha vifo vya watu 17, wengi wao wakiwa wapiganaji, huku kila upande ukidai ushindi.

default

Hali bado si shwari Somalia wengi waendelea kuuawa.

Mapigano yalizuka jana jioni baada ya wapiganaji wa Al shabaab wanaoungwa mkono na kundi la kigaidi la Al Qaeda, kuyashambulia majeshi ya serikali katika mji wa Yet ulioko mpakani mwa Ethiopia.

Hata hivyo habari kutoka katika eneo hilo, zinasema kuwa idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.

Kundi la wapiganaji wa Al Shabaab ambalo pia linadhibiti eneo kubwa la kusini mwa nchi hiyo, limedai ushindi katika mapigano hayo dhidi ya majeshi ya serikali.

Kamanda wa Al Shabaab, katika wilaya ya Hodur, Sheikh Hassan Mohamed amedai kuwa wanadhibiti mji, baada ya kuyashinda majeshi ya serikali.

Hata hivyo wakaazi wa eneo hilo wamesema leo kwamba hakuna uhakika wa nani anadhibiti eneo hilo baada ya mapigano hayo ya jana usiku.

Maafisa wa Jeshi la Somalia wamekiri kuwepo kwa mapigano hayo, lakini wamekana kwa jeshi lao kushindwa na Al Shabaab.

Kundi la Wapiganaji la Al Shabaab na kundi la Hezb al Islam yalianzisha mashambulio ya nguvu Mei 7 mwaka huu, kwa lengo la kuing'oa madarakani serikali inayoongozwa na Rais Sharif Sheikh Ahmed.

Tangu kujitoa kwa majeshi ya Ethiopia nchini Somalia mwezi Januari mwaka huu, wapiganaji wenye msimamo mkali nchini Somalia wamekuwa wakiyalenga Majeshi ya Kulinda amani ya Umoja wa Afrika.

Katika shambulio la kujitoa mhanga lililofanywa na wapiganaji hao, Alhamisi ya wiki iliyopita watu 21, wakiwemo wanajeshi 17 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika waliuawa.

Shambulio hilo ni kubwa kwa kuua wanajeshi wengi wa kikosi hicho, toka majeshi ya Umoja wa Afrika yalipopelekwa huko mwezi Machi mwaka 2007.

Wakati huohuo imeelezwa kuwa Kikosi cha Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Somalia kinahitaji kuimarishwa zaidi.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini Burundi Nicolas Bwakira wakati wa mazishi ya wanajeshi 12 wa Burundi waliouawa nchini Somalia.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Burundi Yves Sahinguvu amesema wanatoa wito kwa Jeshi hilo kuimarishwa zaidi ikiwemo kupatiwa vifaa zaidi na kuwezeshwa kifedha ili kuweza kuvifanya vikosi hivyo kufanya vizuri.

Amesema licha ya idadi hiyo ya wanajeshi wao waliouawa, akiwemo Jenerali Juvenal Niyonguruza hawata kata tamaa, wanajeshi wa Burundi wataendelea kubaki nchini Somalia mpaka watakapomaliza kazi yao kwa msaada wa Jumuia ya Kimataifa, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Burundi na Uganda ndio nchi pekee za Afrika zilizotoa wanajeshi wao nchini Somalia, kama Kikosi cha Jeshi la Kulinda amani cha Umoja wa Afrika.

Mwandishi: Halima Nyanza (afp)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 21.09.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JlTV
 • Tarehe 21.09.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JlTV
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com