1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 100 wauawa katika shambulio la bomu Afghanistan

8 Oktoba 2021

Watu 100 wameuawa na wengine wamejeruhiwa katika shambulizi la kujitoa muhanga leo Ijumaa katika msikiti wa Washia ulioko mjini Kunduz Afghanistan.

https://p.dw.com/p/41SLB
Afghanistan | Anschlag auf eine Moschee in der Provinz Kundus
Picha: Abdullah Sahil/AP Photo/picture alliance

Shambulio hili kwenye msikiti ni baya zaidi kushuhudiwa baada ya kuondoka kwa vikosi vya Marekani.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan kupitia mtandao wa twitter umesema kwamba taarifa za awali zimeashiria kwamba zaidi ya watu 100 wameuwawa na wengine kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa ndani ya msikiti.

Bomu liliripuka katika msikiti wa Gozar-e-Sayed Abad wakati wa sala ya Ijumaa.

Mmoja wa walioshuhudia tukio hilo, Ali Reza, amesema alikuwa anasali wakati ulipotokea mripuko na kuongeza kuwa ameona majeruhi wengi.

Soma pia: Je uvamizi wa Marekani Afghanistan uliibadilisha taifa hilo?

Picha na video za matukio zimeonyesha miili iliyotapakaa kwenye vifusi huku waokoaji wakibeba miili iliyokuwa imefungwa ndani ya blanketi kutoka msikitini hadi katika gari la kubebea wagonjwa. Ngazi za kuingilia msikiti huo zilikuwa zimejaa damu.

Naibu polisi wa mkoa wa Kunduz, Dost Mohammad Obaida, amesema hakuna kundi lolote hadi sasa lililokiri kuhusika na shambulio hilo lakini wanamgambo wa kundi la dola la Kiislamu wana historia ya muda mrefu ya kuwashambulia waumini walio wachache wa Shia.

Mkurugenzi wa utamaduni na habari wa Kunduz kwa serikali mpya ya Taliban nchini Afghanistan, Matiullah Rohani, amelithibitishia shirika la habari la AFP kuwa tukio hilo baya ni shambulio la kujitoa muhanga.

Msemaji wa Taliban Zabuhullah Mujahid vile vile amethibitisha shambulizi hilo la ndani ya msikiti wa waumini wa Shia.

Aminullah mmoja wa walioshuhudia tukio hilo ambaye kakake alikuwa ndani ya msikiti wakati wa shambulio hilo amesema " Baada ya kusikia mlipuko nilimpigia simu kaka yangu lakini hakupokea. Nilitembea kuelekea msikitini na kumpata akiwa amejeruhiwa na amepoteza fahamu. Upesi tulimpeleka hospitali."

Kunduz ni eneo muhimu la ubadilishanaji wa uchumi na biashara kati ya Afghanistan na Tajikistan.