Watoto Milioni 10.5 watumikishwa kazi za majumbani duniani | Masuala ya Jamii | DW | 12.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Watoto Milioni 10.5 watumikishwa kazi za majumbani duniani

Shirika la kazi duniani,ILO limetoa mwito wa kupiga marufuku mtindo wa kuwalazimisha watoto kuwa watumishi wa majumbani.Shirika la ILO limesema hayo katika ripoti yake iliyotolewa mjini Geneva

Watoto wanavyotumikishwa duniani

Watoto wanavyotumikishwa duniani

Shirika la ILO limesema katika ripoti yake kwamba watoto karibu milioni 10.5 duniani wanatumikishwa kazi za nyumbani katika mazingira mabaya.

Katika ripoti hiyo Shirika la Kazi Duniani ,limeeleza kwamba watoto hao wanafanya kazi za usafi, wanapika,wanatunza bustani na pia wanafanya kazi ya uyaya.

Katika ripoti hiyo iliyotolewa kuadhimisha siku ya kupinga kutumikishwa kwa watoto duniani kote, Shirika la ILO limetilia maanani kwamba mamilioni ya watoto wanafanyishwa kazi katika mazingira ya hatari na ya utumwa.

Wengi ni watoto sana:

Asasi hiyo imesema katika ripoti yake kuwa watoto milioni sita na nusu wanaofanyishwa kazi za majumbani wana umri kati ya miaka 5 na 14 na zaidi ya asilimia 71 ni wasichana. Hata hivyo asasi ya ILO imeeleza kuwa ni vigumu kuwalinda watoto hao. ILO imesema ,pamoja na kutumikishwa ndani ya nyumba za waajiri wao katika mazingira ya faragha,jamii zao haziwezi kuziona kazi ambazo hasa wanazifanya. Watoto hao aghlabu hutenganishwa na familia zao na kujikuta katika mazingira ya kuwategemea waajiri wao na hivyo kunaswa.

Wanyanyaswa kijinsia:

Shirika la kazi duniani ILO limesema kuwa watoto wengi wanaoajiriwa majumbani mara nyingi hawalipwi na waajiriwa wao. Pamoja na hayo watoto hao wanabaguliwa. Shirika la kazi duniani pia limeeleza katika ripoti yake kwamba, kutokana asili ya kazi wanayozifanya ,watoto hao wanakuwamo katika hatari ya kufanyiwa vitendo vya nguvu na kunyanyaswa kijinsia na waajiri wao.

Katika ripoti yake shirika la ILO limemnukulu msichana mmoja mwenye umri wa 14 kutoka Togo akisema ingelikuwa bora kwa waajiri wao kuwapa ushauri na kuwapa maadili, badala ya kuwapiga,kuwatesa, kuwaumiza kwa tumia nyembe na kuwatia pilipili katika sehemu zao za siri. Msichana huyo ameliambia shirika la ILO kwamba wakati mwingine waajiri wake walimnyima chakula.

Mahitaji ya watumishi wa nyumbani yaongezeka:

Mahitaji ya wafanyakazi za nyumbani yanaongezeka duniani kutokana na wanawake wengi kupata kazi nje ya nyumba zao na pia kutokana na kuzidi kuzeeka kwa watu wanaohitaji kuhudumiwa.

Shirika la kupinga utumwa duniani lenye makao mjini London, "Anti Slavery International" limewahoji watoto 400 waliowahi kufanya kazi za utumishi wa nyumbani pamoja na wale ambao bado wanaendelea kuzifanya kazi hizo.

Watoto hao kutoka Costa Rica hadi Ufilipino wamesema jambo muhimu sana kwao ni kuunganishwa tena na familia zao.Pia wamesema muhimu ni kurejea shuleni. Aidha wamesema kwamba itafaa ikiwa wahusika wataingilia kati ili kutetea haki za watoto hao na kuziimarisha jumuiya za wafanyakazi,za watumishi wa majumbani.

Hali ni ya kutia wasi wasi Afrika:

Katika ripoti yake shirika la ILO limearifu kuwa hali ni ya kuyatia wasi wasi katika nchi kama Burkina Faso,Ghana ,Mali na Ivory Coast

Mkurugenzi wa mpango wa shirika la ILO wa kuutokomeza "ujakazi" wa watoto duniani Constance Thomas amesema hali ya watoto wengi wanaofanya kazi ya utumishi wa nyumbani inasababisha siyo tu kukiukwa kwa haki za watoto bali ni kizingiti kikubwa cha maendeleo duniani.

Mwandishi: Mtullya Abdu/dpa,afpe,

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com