1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watanzania hatarini kupigwa marufuku kusafiri Marekani

Iddi Ssessanga
22 Januari 2020

Utawala wa Rais Donald Trump unapanga kuongeza mataifa saba kwenye orodha ya mataifa ambayo raia wake hawaruhusiwi kuingia nchini Marekani. Miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na Nigeria, Sudan, Eritrea na Tanzania.

https://p.dw.com/p/3WeKa
USA Reisen Flughafen Washington
Picha: Getty Images/AFP/P.J. Richards

Rais Donald Trump alisema katika mahojiano na gazeti la Wall Street Journal kwamba alikuwa anafikiria kuongeza mataifa kadhaa kwenye orodha ya marufuku ya kusafiri Marekani, lakini alikataa kuyataja hasa mataifa hayo.

Lakini siku ya Jumannne, vyombo vya habari nchini humo vikatoa rodha ya mataifa yanayozingatiwa kuongezwa kwenye orodha hiyo ambayo ni Belarus, Eritrea, Kyrgyzstan, Myanmar, Nigeria, Sudan na Tanzania.

Baadhi ya mataifa yatawekewa marufuku kwenye baadhi ya kategoria za visa, kwa mujibu wa Wall Street Journal na kulingana na tovuti ya Politico, orodha hiyo haikuwa ya mwisho na huenda ikabadilishwa tena. 

Afisa mwandamizi katika utawala wa Trump alisema mataifa yalioshindwa kutekeleza masharti ya kiusalama, ikiwemo alama za vidole, ushirikishaji wa taarifa na hatua za kukabiliana na ugaidi, yanakabiliwa na hatari ya vikwazo vya idara ya uhamiaji ya Marekani.

Einweihung eines neuen Flugahfen Terminals durch John Pombe Magufuli  Kassim Majaliwa
Eneo jipya la wasafiri katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam.Picha: DW/ E. Boniphace

Hatari ya kuvuruha uhusiano na mataifa husika

Hatua hiyo ya Marekani huenda ikatia doa pia uhusiano wa nchi hiyo na mataifa mengi yalioathiriwa na upanuzi wa marufuku hiyo.

Nigeria kwa mfano, taifa kubwa zaidi kiuchumi barani Afrika na linaloogoza kwa wakaazi wengi, ni mshirika wa Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi na ina raia wake wengi wanaoishi nchini Marekani.

Wizara ya mambo ya ndani ya Marekani haikujibu maombi ya kutoa tamko kuhusiana na taarifa hizo, na wizara ya mambo ya nje ilikataa kuzungumzia suala hilo.

Chini ya marufuku ya sasa, raia wa Iran, Libya, Korea Kaskazini, Somalia, Syria na Yemen pamoja na baadhi ya maafisa wa serikali ya Venezuela na ndugu zao wamezuwiwa kuingia nchini Markeani.

Chad iliwekwa kwenye orodha hiyo awali lakini iliondolewa Aprili 2018. Raia wa mataifa yalioorodheshwa wanaweza kuomba msamaha dhidi ya marufuku hiyo lakini hili hufanyika kwa nadra sana.

Chanzo: rtre