1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watalamu wa matibabu waelezea mashaka kuhusu Olimpiki

Bruce Amani
20 Aprili 2020

Michezo ya Olimpiki ya Tokyo Julai mwaka ujao itakuwa ni tukio la hatari ya kipekee, likihitaji ushirikiano kutoka kwa waandalizi wakati kukiwa na sintohafamu kutokana na janga la virusi vya corona

https://p.dw.com/p/3bBLz
Japan Tokio Olympische Spiele verschoben  "Tokyo 2021"
Picha: Reuters/D. Ruvic

Japan na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki walifanya uamuzi usio wa kawaida mwezi jana kuchelewesha michezo hiyo kwa mwaka mmoja, wakati ulimwengu ukipambana na virusi hivyo ambavyo vimewaambukiza watu milioni 2.3 na kuwauwa zaidi ya 150,000 kote duniani. Lakini maswali bado yapo kama Michezo hiyo inaweza kufanyika miezi 15 kutoka sasa, kwa sababu chanjo huenda ikapatikana mwaka mmoja kutoka sasa. Zach Binney ni mtalaamu wa magonjwa ya mlipuko katika Chuo Kikuu cha Emory nchini Marekani "Tunapozungumzia kurejesha michezo na mashabiki kufurika viwanjani, nadhani hicho ni kitu tutahitajika kusubiri kabla ya chanjo kufanya kazi na hiyo huenda ikachukua angalau mwaka mmoja na nusu kutoka wakati ambao mlipuko ulianza, kwa hiyo tunazungumzia kama ni mapema zaidi, mwishoni mwa 2021"

Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 itaanza Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka ujao, lakini waandalizi wanatarajia mabadiliko machache kwa mpango wa awali, ikiwemo uhudhuriaji wa mashabiki. Binney anasema itakuwa hatari sana kwa sababu wageni watatoka kote ulimwenguni yakiwemo maeneo yenye maambukizi mengi.

Jason Kindrachuk, mtalaamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka Chuo Kikuu cha Manitoba Canada, anasema kuna hatari ya kucheleweshwa Michezo hiyo hata zaidi, kwa sababu kuwapa watu chanjo huchukua muda "Sio tu kuhakikisha kuwa kila mtu amepewa chanjo, lakini pia uhakikishe kuwa chanjo hiyo imetolewa na kuwa kinga ya mwili ya wanaliopewa inakabiliana vizuri na chanjo hiyo. Na haustahili kuwapa watu chanjo wakati wa Olimpiki, bali mapema kiasi kabla ya kuanza ili waijenge hiyo kinga bora ya mwili." Dr Kentaro Iwata, profesa wa magonjwa ya kuambukiza katika Chuo Kikuu cha Kobe nchini Japan, yeye ameelezea mashaka makubwa kama kweli Japan itakuwa tayari mwaka ujao. "Japan huenda ikaudhibiti ugonjwa huu kufikia msimu wa joto mwaka ujao, na natumai kuwa tungeweza, lakini sidhani hilo litawezekana kwngineko duniani. Kwa hiyo, nina mashaka sana kuhusu kuandaa michezo ya Olimpiki msimu wa joto mwaka ujao, isipokuwa kama utaandaa michezo hiyo katika muundo tofauti kabisa kama vile bila mashabiki, au uhudhuriaji mdogo sana.

Kamati ya maandalizi ya Tokyo 2020 hata hivyo imejibu ikisema kuwa kuwa inalenga kikamilifu katika kufanikisha Michezo hiyo mwaka ujao. Msemaji wa kamati hiyo Masa Takaya ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kwa sasa hawaoni kama ni vyema kujibu maswali ya kubahatisha