1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WaSrilanka waandamana kumtaka Rais aitishe vikao vya Bunge

30 Oktoba 2018

Raia wa Sri Lanka wameandamana kumshinikiza Rais Maithripala Sirisena kuitisha kikao cha Bunge mara moja ili kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo

https://p.dw.com/p/37OQJ
Sri Lanka Protest von Unterstützern des abgelösten Ministerpräsidenten
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Jayawardena

Zaidi ya watu elfu kumi wakiwemo wabunge na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wameandamana mjini Colombo, wakiimba nyimbo mbalimbali wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe unaosema, ''Tuushinde udikteta unaoidhoofisha katiba, turejeshe demokrasia, zingatia katiba na bunge lirejelee vikao ili tusitishe mgogoro´´. Baadaye walifanya mkutano karibu na nyumba ya waziri  mkuu.

Maandamano hayo yanajiri siku moja baada ya ya Spika wa Bunge Karu Jayasuriya kuonya kuwa huenda kukashuhudiwa ghasia iwapo wabunge hawatarejea bungeni mara moja. Rais Sirisena alimfuta kazi Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe na baraza lake la mawaziri Ijumaa wiki iliyopita na kumteua Mahinda Rajapaksa kuchukua wadhifa huo.

Sri Lanka Protest von Unterstützern des abgelösten Ministerpräsidenten
Wafuasi wa Wickremesinghe wakiimba nyimbo wakati wa maandamano nje ya makao rasmi ya Waziri Mkuu huyo aliyefutwa kaziPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Jayawardena

Wickremesinghe anataka vikao vya bunge virejelewe akisema ana uungwaji mkono wa idadi kubwa ya wabunge. Jumamosi iliyopita, Oktoba 27, Rais Sirisena alisitisha vikao vya Bunge ikiwa ni njia mojawapo ya kumpa Rajapaksa muda wa kupata uungaji mkono wa kutosha ili asikabiliwe na kura ya kutokuwa na imani naye.

Hatua ya Rais Sirisena kumfuta kazi waziri mkuu imetajwa na baadhi ya waangalizi kwamba itazua mgogoro ya kikatiba. Siku ya Jumapili, watu wawili waliuawa na mwingine mmoja kujeruhiwa baada ya ufyatulianaji risasi katika ofisi ya Wizara ya Mafuta, tukio ambalo linadaiwa kusababishwa  na mgogoro huo.

Sri Lanka Unterstützer des abgesetzten Premierminister Ranil Wickremesinghe vor dessen offiziellen Wohnsitz in Colombo
Wafuasi wa Waziri Mkuu aliyefutwa kazi Ranil Wickremesinghe wakisubiri nje ya makao yake rasmi mjini Colombo, Sri LankaPicha: Reuters/D. Liyanawatte

Marekani imesema inafuatilia matukio nchini Sri Lanka huku ikimtaka Rais Sirisena kuitisha vikao vya Bunge. Rais huyo alisema amemfuta kazi Wickremesinghe kutokana na madai ya kuhusika kwa waziri mmoja katika mpango wa kutaka kumuua. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo. Wickremesinghe amekanusha madai hayo.

Wafuasi wa Rais Sirisena wamekuwa wakiuzungumzia mpango huo kwa wiki kadhaa, lakini jana rais akauzungunzia hadharani. Polisi wanaendeleza uchunguzi wa madai hayo lakini hakuna aliyekamatwa kwa kuhusishwa na suala hilo.

Wakati uo huo, wafuasi wa Rajapaksa ambaye ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Sri Lanka wanamtaka Wickremesinghe aondoke katika makazi yake rasmi, la sivyo wamuondoe kwa nguvu.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE

Mhariri: Saumu Yusuf