Wasomalia wamesahaulika asema mjumbe maalum wa UN Somalia | Habari za Ulimwengu | DW | 21.03.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

Wasomalia wamesahaulika asema mjumbe maalum wa UN Somalia

-

NEW-YORK

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limefanya kikao maalum hapo jana cha kutafakari uwezekano wa kuongeza hatua za kujihusisha kwa Umoja wa mataifa katika taifa la Somalia linalokabiliwa na mgogoro.Hata hivyo wanachama muhimu kwenye baraza hilo wameondoa uwezekano wa kupelekwa haraka kikosi kamili cha kuweka amani cha Umoja huo nchini humo.

Baraza la usalama lenye wanachama 15 liliarifiwa kwa mukhtasari juu ya hali ya mambo nchini Somalia na mjumbe wake maalum katika taifa hilo Ahmedou Ould Abdallah ambaye anasema nchi hiyo imetelekezwa kwa muda mrefu na kwamba wasomali wanaendelea kuadhibiwa kutokana na kushindwa kwa ujumbe wa kuweka amani wa Umoja wa mataifa katika miaka ya tisini.Bwana Ould ameendelea kuusihi Umoja wa Mataifa kwamba usiitupe mkono Somalia na wala usiwaadhibu wale wasiohusika na vita au wale ambao hawakuhusika miaka ya tisini wakati wakubwa zao walipofanya makosa dhidi ya jumuiya ya kimataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa lilijadiliana juu ya masuala manne yaliyopendekezwa na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon katika ripoti yake juu ya taifa hilo.Mjumbe maalum wa SomaliaOuld Abdalla amesema kitengo kinachohusika na opresheni za amani cha Umoja huo kinapanga kutuma ujumbe mpya nchi humo mwezi ujao.Hata hivyo balozi wa Uingereza katika Umoja wa mataifa John Sawers amesema ipo nafasi ya kupiga hatua lakini inabidi kwanza hali ya kisiasa iimarishwe katika taifa hilo vinginevyo itakuwa vigumu wanajeshi wa Umoja wa mataifa kupelekwa Somalia.

Kwa sasa kuna wanajeshi kiasi 2300 kutoka Burundi na Uganda wa kikosi cha Umoja wa Afrika na mauaji bado yanaendelea,jana watu sita waliuwawa kwenye mapigano kati ya wanajeshi wa Somalia na wanamgambo kusini mwa mji mkuu Mogadishu.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com