Wasomali wengi wakimbilia Kenya | Masuala ya Jamii | DW | 29.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Wasomali wengi wakimbilia Kenya

Idadi ya Wasomali wanaokimbia vita na ukame katika nchi yao na kuingia Kenya inazidi kupanda. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa, Wasomali wapatao 1,300 huyaacha makazi yao na kukimbilia nchini Kenya kila siku.

default

Wakimbizi kutoka Somalia katika kambi nchini Kenya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limesema kwamba idadi kubwa ya wakimbizi hao ni wakulima na wachunga mifugo ambao mashamba yao yamekauka na mifugo yao kufa kwa kukosa maji.

Umoja wa Mataifa unaeleza kwamba idadi ya wakimbizi kutoka Somalia imepanda kwa kasi tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Kati ya Januari na Juni mwaka huu, idadi yao inakadiriwa kuwa 55,000. Wakimbizi hao hupokewa katika kambi ya Dadaab iliyoko Kaskazini mwa Kenya,  na iliyojaa kupita kiasi. Ikiwa na wakimbizi wapatao 360,000, kambi hiyo ya Dadaab ni ya kwanza kwa ukubwa duniani. Hata hivyo shirika la UNHCR limesema kwamba limeshindwa kutoa viwanja vipya kwa ajili ya wakimbizi hao na hivyo inabidi baadhi yao wakae nje ya kambi hiyo.

Somalische Flüchtlinge in Kenia

Wakimbizi wa Kisomali wakicheza nje ya kambi ya Dadaab.

"Kuna kambi ambayo tulikuwa tuijenge lakini serikali imetuambia tusubiri kidogo ili ione kama itaturuhusu kupeleka wakimbizi hapo," anaeleze Emmanuel Nyabera, msemaji wa shirika hilo jijini Nairobi.

Shirika la UNHCR limeripoti kwamba, Wasomali 750,000 wameikimbia nchi yao kutokana na mapigano na shida zinazoendelea Somalia.

Vile vile watu Millioni moja na nusu wameyakimbia makaazi yao lakini bado wamebaki Somalia.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yamekuwa yakiendelea Somalia kwa muda wa miaka 20 sasa. Serikali ya mpito isiyo na nguvu lakini inayotambuliwa kimataifa imeshindwa kuudhibiti mji mkuu Mogadishu na sehemu nyengine  za Somalia. Ikisaidiwa na majeshi ya Umoja wa Afrika, serikali ya Somalia inapigana dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu mabao kwa kiwango fulani wana mawasiliano na kundi la kigaidi la al-Qaeda.

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com